23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Simbachawene apongeza wananchi Kibakwe kwa kujenga shule ya kisasa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene amewapongeza Wananchi wa Kata ya  Lumuma jimboni humo kwa kazi kubwa waliyoifanya ya  kujenga  Shule ya Sekondari ya Lumuma Green kwa nguvu zao wenyewe ambayo ina wanafunzi 106  wa kidato cha kwanza kutoka vijiji vitatu vinavyounda Kata hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene akizungumza na Wananchi wa Kata ya  Lumuma mara baada ya kutembelea  shule iliyojengwa kwa nguvu za wananchi wa jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma

Ametoa Pongezi hizo wakati akizungumza na Wananchi kwa nyakati tofauti katika vijiji  vya Lufusi, Kitati na Lumuma Mafene Kata ya Lumuma kupitia mikutano ya hadhara anayoendelea kuifanya katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Amesema amefurahishwa na uthubutu na utayari uliooneshwa na wananchi wa Kata hiyo kwa kukubali kuunganisha nguvu zao kwa  pamoja katika kukamilisha shule hiyo yenye majengo ya kisasa.

Amesema Serikali inavutiwa na uongozi wenye maono na mtazamo wa kimapinduzi kwa kuanza kusaidia pale nguvu za wananchi zilipoishia ili kuistawisha jamii hiyo.

Amemtaja Diwani wa Kata hiyo, Jocktan Cheligah kama Kiongozi mwenye uthubutu na mbunifu ambaye amedhamiria kuhakikisha shule  hiyo inajengwa ili wanafunzi wa vijiji hivyo wanapata elimu katika mazingira rafiki.

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene ameahidi kusaidia kujenga nyumba pacha tatu kwa ajili ya kuwasaidia walimu ambao wanaishi mbali na eneo la shule.

Amesema akiwa ndiye Mbunge wa jimbo lao la Kibakwe, anahitaji wananchi wanaoonesha njia ili Serikali iweze kusaidia kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

‘’Kwa kujenga shule hii, mimi binafsi mmenitia moyo, hivyo naomba niwaahidi kuwa nitahakikisha hadi kufika mwakani tunakuwa na majengo mengi zaidi ili watoto wetu wasome katika mazingira bora,’’ amesisitiza Simbachawene.

Amefafanua kuwa, nguvu za wananchi zinahitajika ili kuhakikisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kwani Serikali ina vipaumbele vingi hivyo bila wananchi wenyewe kuanza kubuni miradi hiyo huwa ngumu kuitekeleza miradi hiyo kwa wakati.

Katika hatu nyingine, Simbachawene ameridhishwa na mradi wa ujenzi wa zahanati ulioibuliwa na wananchi wa Kijiji cha Lufusi na kuahidi kuwa ataisaidia katika ukamilishaji wa Zahanti hiyo kwa wakati.

‘’Naomba niwaahidi kuwa, kuptia mfuko wa Jimbo na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tutahakikisha fedha zinapatikana ili kusaidia katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa zahanati hiyo mliyoanza.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, George Fuime ameahidi kutenga fedha za kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo kwa nia ya kuunga mkono shughuli zinazofanywa na wananchi wa Kata hiyo.

“Tutahakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuunga nguvu za wananchi katika masuala ya maendeleo yaliyobuniwa na wananchi wenyewe, amesema Mhe. Fuime.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Jocktan Cheligah ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Simbachawene kwa utayari wake wa kukubali kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi anaowaongoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles