Na Mwandishi Wetu- Dodoma
SERIKALI imeziagiza halmashauri, miji na majiji nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (LGTI).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, amesema hivi karibuni kuwa Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Hombolo) kipo mahususi kwa kutoa mafunzo kwa ajili ya wafanyakazi wanaoajiriwa kwenye Serikali za mitaaa nchini.
“Naagiza kunapokuwa na nafasi za kazi kwenye halmashauri, miji na hata majiji ni vyema wahitimu wa chuo hiki wakapewa kipaumbele. Ni vizuri wakapata nafasi ya kushindanishwa na wengine kwani hawa ni walengwa,” alisema Waziri Simbachawene wakati alipokutana na viongozi na wawakilishi wa chuo hicho mjini Dodoma.
Waziri Simbachawene aliuagiza uongozi wa chuo hicho kutosita kutoa taarifa yoyote endapo chuo kinapokuwa na upungufu wa watumishi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Martin Madale, alimshukuru Waziri Simbachawene kwa kuwa karibu na chuo na pia kufuatilia maendeleo na ustawi.
“Kwa niaba ya bodi, menejimenti, wafanyakazi na wanachuo wote wana imani kubwa na uongozi wako kwani umekuwa karibu sana nasi na pia umekuwa msaada mkubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo,” alisema Dk. Madale.
Alimwomba waziri kukisaidia chuo kupata kompyuta zaidi, viti na vifaa mbalimbali ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoomba kujiunga na chuo hicho kwa sasa.