Simba yatua Dar, hasira zao zote kwa Mbeya City

0
1028

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Simba kimetua jana Dar es Salaam kutoka Shinyanga na kuanza mara moja maandalizi ya kumaliza hasira zao za kufungwa na Mwadui watakapokutana na Mbeya City Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini.

Simba ilifungwa na Mwadui FC bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kikosi hicho kilifika Dar es Salaam jana asubuhi ambao leo asubuhi wataendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru, kujiandaa na mchezo huo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema, baada ya kufika Dar es Salaam, wanaendelea na mazoezi kujiweka fiti kuivaa Mbeya City.

“Tumefika salama (Dar es Salaam) tukitokea Shinyanga, tumewapa ruhusa wachezaji waende nyumbani, lakini kesho (leo) asubuhi tutaendelea na mazoezi na kuingia kambini kabisa kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City Jumapili,” alisema.

Alisema wachezaji wote waliosafiri na timu wapo salama hivyo kwa sasa wanautizamia mchezo huo dhidi ya Mbeya City.

Simba watakutana na Mbeya City wakiwa na kumbukumbu ya kuifunga mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na waliporudiana Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Wekundu wa Msimbazi hao walishinda mabao 2-1.

Simba itahitaji kufanya vizuri katika mchezo huo ili iendelee kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo baada ya kutoka kupoteza dhidi ya Mwadui FC.

Wachezaji wa Simba waliokuwa majeruhi ambao wanaendelea na mazoezi mepesi ni Jonas Mkude, John Bocco na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ pamoja na Shomary Kapombe aliyekuwa anaumwa malaria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here