25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yashindwa kuitambia URA

Pg 32

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya URA katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo zilianza mchezo kwa kushambuliana kwa zamu huku kila mmoja akitafuta nafasi ya kushinda.

Katika mchezo huo, URA walianza kuifunga Simba katika dakika ya 19 kupitia kwa Nkugwa Elkanah, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kagimu Shafiq.

Bao hilo liliishtua safu ya ushambuliaji ya Simba inayonolewa na kocha Joseph Omog ambapo katika dakika ya 26, Wekundu hao wa Msimbazi walikosa bao baada ya Jamal Mnyate kupiga shuti lililotoka nje.

Simba iliendelea kulisakama lango la URA na mashambulizi hayo yalizaa matunda katika dakika ya 32, baada ya Jonas Mkude kuisawazishia timu yake, akiunganisha faulo iliyopigwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Simba baada ya kusawazisha bao hilo, ilizidi kuliandama lango la URA na katika dakika ya 42 mshambuliaji wake, Shiza Kichuya alipiga shuti lililookolewa na beki wa URA na hivyo timu hizo kwenda mapumziko wakiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa URA kuliandama lango la Simba ambapo katika dakika ya 58, mshambuliaji wa timu hiyo, Sekoti Sam, alikosa bao la wazi akiwa na kipa Vicent Angban.

Hata hivyo, katika dakika ya 84 Simba ilikosa bao baada ya mshambuliaji wake, Fredrick Blagnon, kupokea mpira kutoka kwa Mussa Ndusha.

Licha ya mashambulizi ya hapa na pale, hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Katika mchezo huo, Simba waliutumia pia kumuaga nahodha wao, Mussa Hassan ‘Mgosi’, ambaye alizunguka uwanjani akiwapungia mkono mashabiki baada ya  kustaafu rasmi kucheza soka kutokana na kuteuliwa kuwa meneja wa timu hiyo.

Simba: Vicent Angban, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hamad Juma, Novat Lufunga, Metgot Mwanjali, Jonas Mkude, Chiza Kichuya/Haji Gumbo, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib/Fredrick Blagnon, Mussa Mgosi/Jamal Mnyate.

URA: Agaba Oscar, Muwanga Mathias, Sekito Sam, Kawoya Fahad, Kulaba Jimmy, Kagimu Shafiq/Kagaba Nicholas, Lule Jimmy/Wananyaka Richard, Feni Ali, Bokota Labama, Ntambi Julius na Nkugwa Elkanah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles