25.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

SIMBA, YANGA ZAKWAA VISIKI

WAANDISHI WETU

TIMU ya Simba na Yanga, zimeshindwa kutamba baada ya kulazimishwa suluhu katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana katika viwanja tofauti.

Simba ilishindwa kuvuna pointi tatu mbele ya  Ndanda, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Nagwanda Sijaona, Mtwara.

Yanga nayo ilishindwa kufurukuta mbele ya Biashara United, baada ya kulazimishwa suluhu Uwanja Karume, Mara.

Sare hiyo inaifanya Simba kufikisha pointi 80, baada ya kucheza michezo 33, ikishinda 25, sare tano na kupoteza mitatu.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 61, ilizovuna baada ya kucheza michezo 33, ikishinda 16, sare 12 na kupoteza nne.

Yanga imejiweka pabaya kwani, inaweza kuenguliwa katika nafasi ya pili na washindani wao wa karibu, Azam ambao jana usiku walitarajiwa kuumana na  Singida United ambayo inakamata mkia na tayari imeshuka daraja.

Azam ikishinda mchezo huo itafikisha pointi 62.

Timu hizo zimeshindwa kutamba ugenini, ikiwa  ikiwa imebaki wiki moja kabla ya kukutana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, utakaochezwa Jumapili hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kabla ya timu hizo kuumana, Simba itakuwa na kibarua cha kuikabili Namungo, katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Ruangwa, Lindi, huku Yanga ikiikabili Kagera Sugar.

Simba iliuanza mchezo wa jana kwa kumiliki mpira na kucheza pasi nyingi hasa eneo la katikati ya uwanja.

Ndanda kwa upande wao, ilianza kuisoma Simba huku ikitumia mipira mirefu kufika katika lango la wapinzani wao.

Dakika ya 14, mlinda mlango wa Ndanda, Ally Mustafa alifanya kazi nzuri kuokoa mchomo hatari wa John Bocco.

Dakika ya 17, Luis Miquissone alipoteza nafasi ya kuindikia Simba bao, baada ya  kupokea pasi safi ya Bocco, lakini mkwaju wake haukulenga lengo.

Dakika ya 29, Mustafa alifanya kazi nyingine nzuri  ya kupangua shuti kali lililopigwa na Miquissone, kabla ya walinzi kuondosha mpira huo ndani ya eneo la hatari.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa.

Kipindi cha pili kilianza kwa Ndanda kuingia uwanjani na nguvu zaidi kwa lengo la kusaka bao.

Dakika ya 50, Kennedy Juma wa Simba alilimwa kadi ya kadi ya njao, baada ya kumkwatua Omary Mponda wa Ndanda.

Dakika  ya 56, mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula alifanya kazi ya ziada kupangua michomo miwili iliyopigwa, mmoja ukiwa wa kichwa uliopigwa na Mponda na kiki ya Abdul Hamis.

Dakika ya 66, Simba ilifanya mabadiliko, alitoka Pascal Wawa na nafasi yake kuchukuliwa na Erasto Nyoni.

Pia dakika ya 69, aliingia Meddie Kagere kuchukua nafasi ya Bocco kabla ya Gerson Fraga kutoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mzamiru Yassin dakika ya 72.

Kocha wa Ndanda, Abdul Mingange alifanya mabadiliko dakika ya 75, alimtoa Mponda na kumwingiza Omary Ramadhani kabla ya dakika ya 81 kumtoa Vitalisi Mayanga na kumwingiza Hussein Javu.

Dakika ya 83, Javu alilimwa kadi ya njano baada ya kumkwatua Jonas Mkude.

Dakika ya 90, Ndanda ilifanya mabadiliko aliingia Kassim Mdoe kuchukua nafasi ya Kigi Makassy.

Pamoja na mabadiliko ya kila upande dakika 90 zilikamilika kwa suluhu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,528FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles