30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA WANAVYOUKOSA UTAJIRI KWA AJIB NA NIYONZIMA

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

AGOSTI 9, mwaka jana, mashabiki wa klabu ya Manchester United walipata habari njema, kwamba mchezaji wao wa zamani, Paul Pogba, ambaye alikuwa anakipiga katika klabu ya Juventus, amekubali kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.

Mchezaji huyo alisajiliwa na United kwa ada ya uhamisho inayofikia pauni milioni 89 na kusaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia timu hiyo ya ‘Mashetani Wekundu’.

Licha ya Pogba kutokuwa na hadhi hiyo, alivunja rekodi iliyowekwa na Real Madrid mwaka 2009, ilipomsajili Cristiano Ronaldo kwa dau la pauni milioni 80.

Lakini wataalamu wa biashara ndani ya klabu ya Manchester United hawakulifikiria hilo na wala hawakuwa na lengo la mchezaji huyo kuisaidia klabu hiyo.

Kikubwa ambacho wanakiangalia mchezaji akisajiliwa ni wawe na uwezo wa kuuza jezi yake kwa mashabiki, sasa kwa upande wa Pogba, ambaye amesajiliwa kwa pauni milioni 100, hadi sasa fedha hiyo imerudi kutokana na mauzo ya jezi yake.

Baada ya kutambulishwa rasmi na jezi namba yake 6 kuanza kuuzwa kwa wiki tatu za mwanzo tangu amejiunga na United, mauzo ya jezi hiyo kwa kipindi hicho yalifikia zaidi ya pauni milioni 200, huku timu hiyo ikiwa imemnunua kwa pauni milioni 89.

Hii inaonesha ni jinsi gani watu wanajua biashara, kwa kuwa United hawakuangalia ni jinsi gani mchezaji huyo ataweza kutoa mchango wake katika kikosi hicho katika michezo yao, lakini walichokiangalia ni kwamba, hata kama wangemnunua kwa kiasi cha pauni milioni 150, bado United ingekuwa na faida kubwa kwa mauzo ya jezi yake.

Hata PSG walitumia kigezo kama hicho kumsajili Neymar kwa sababu hii, Neymar ni chapa kubwa kibiashara kwa sasa baada ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Matajiri wa PSG wanajua kuwa wakimnasa Neymar watafanya biashara kubwa kupitia mauzo ya jezi yake, pia itavutia kampuni zaidi kumwaga fedha ndani ya klabu hiyo kutokana na uwepo wa staa huyo.

Licha ya ufundi mkubwa wa kuuchezea mpira alionao Neymar, pia kijana huyo wa Kibrazil ana mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka duniani kutokana na kuwa na wafuasi milioni 78.7 katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

Ukiangalia katika soka la Tanzania stori ni tofauti kidogo, huku hakuna watu wanaoumiza vichwa kufanya tathmini kama hizi kabla ya kufanya usajili wa wachezaji katika klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tanzania kila klabu ikisajili utasikia tunasajili kwa ajili ya kuboresha kikosi cha msimu ujao wa Ligi Kuu au michuano ya kimataifa kama zilivyo Simba na Yanga.

Agosti Mosi mwaka huu, Simba ilitangaza kumnasa kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima, huku nao wakijibu mapigo kwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib, aliyekulia Msimbazi, japo wao walimtangaza mapema kidogo.

Nyuma ya sajili hizi mbili, kuna utajiri mkubwa umejificha katika mauzo ya jezi mpya za mastaa hao kwenye timu zao mpya kwa msimu ujao, kutokana na wachezaji hao wote kuwa vipenzi vya mashabiki wa soka nchini.

Tofauti kubwa ya soka la Tanzania na nchi nyingine zilizoendelea, itaanza kuonekana muda si mrefu, wenzetu wako makini ndani na nje ya uwanja.

Simba imemwaga fedha kibao kumshawishi Niyonzima kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo, Yanga nao wamepigana kufa na kupona kuipata saini ya Ajib, ila wanachosahau Simba na Yanga kuwa wachezaji hao wanatakiwa kuwa chanzo cha kuvuna fedha.

Wachezaji hao wana ushawishi mkubwa wa mashabiki wa soka nchini, kutokana na viwango vyao, hakuna mjadala juu ya Ajib alivyokuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba,  wataalamu wa masoko wa Yanga wanaweza kutumia mwanya huo kwa kuingiza fedha katika jezi zake ili kuwaumiza wapinzani wao.

Simba pia wanatakiwa kuwa ‘busy’ kufanya biashara ya kuuza jezi za Niyonzima, ambaye aliichezea Yanga kwa misimu sita mfululizo kwa kiwango cha juu, Simba wakiwa makini wanaweza kuwarusha roho Yanga kwa kuuza kwa wingi jezi ya kiungo huyo, ambaye mashabiki wa Yanga walichoma jezi yake baada ya kusikia hawatakuwa naye katika kikosi.

Biashara hizi zinawezekana kufanyika kutokana na klabu hizo kuwa na mashabiki na wanachama wengi kuliko nyingine zote Tanzania, labda klabu zenyewe zishindwe kutumia fursa hiyo.

Timu hizo zikishindwa kutengeneza fedha kupitia majina ya wachezaji hao msimu ujao, itabidi zijilaumu zenyewe, kwani mauzo ya wachezaji hao kwa kipindi cha mwezi mmoja yanaweza kurejesha fedha zao walizosajiliwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles