23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA, SINGIDA MTAJUTIA KUWAKOSA EVERTON

NA MARTIN MAZUGWA


MCHEZO wa soka umekuwa biashara ambayo imekuwa ikiwatoa vijana wengi katika kundi la umasikini na kuwapa maisha mazuri, mfano Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Alexis Sanchez, Gabriel Jesus  na wengine wengi ambao hivi sasa wamekuwa wakiogelea fedha kupitia mchezo wa soka.

Wakati mataifa mengine yakizidi kuwekeza zaidi katika biashara hii ambayo imekuwa ikiiongezea kipato nchi, hali ni tofauti nchini Tanzania ambapo badala ya kuamka tumeamua kulala na kuiacha nafasi hii adimu kwa vijana wetu.

Kati ya mambo ambayo tunapaswa kujutia basi ni kitendo cha klabu zetu za Simba, Yanga pamoja na Singida United kushindwa kupambana katika fainali ya Sportpesa na kuwaacha Gor Mahia kutoka  Kenya wakitwaa ubingwa wa michuano hiyo na hatimaye kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Everton.

Kitendo cha kushindwa kuyapa uzito mashindano ya Sportpesa yaliyofanyika hapa nchini, hakika ni uzembe ambao unapaswa kukemewa zaidi ili usijirudie.

Kushindwa kucheza na Everton timu inayoshika nafasi ya saba katika Ligi Kuu ya England EPL ambayo pia itacheza hatua ya mtoano wa Europa, wachezaji wetu wamekosa  kitu muhimu sana.

Ilikuwa ni nafasi ya vijana wetu kuonyesha vipaji vyao kupitia mchezo huo ambao ulitazamwa duniani kote kutokana na ukubwa wa klabu ya Everton yenye historia ya kipekee kutoka Merseyside, England.

Kitendo cha kuwaacha Wakenya waonekane kimataifa kimeongeza thamani ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL), kimataifa kwani naamini uwezo ulioonyeshwa na vijana wa Gor Mahia ambao walionyesha kandanda safi tayari wamejiuza nje ya mipaka ya nchi yao.

Mbali na kuitangaza Ligi Kuu ya Kenya, lakini pia tayari wasifu wa nyota wa  Gor Mahia umeongezeka kutokana na kucheza mchezo huo na Everton, kwani ni nadra sana kuona timu kubwa  kutoka barani Ulaya hususan England kuja Afrika kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hususani Tanzania kupokea klabu kubwa yenye mashabiki wengi ulimwenguni kama Everton.

Ingawa ilikuwa mwisho wa msimu, klabu zetu hazikupaswa kuyadharau mashindano haya, ilihitaji kuyatumia kama maandalizi ya michuano ya kimataifa kutokana na klabu za Simba na Yanga mwaka huu kuiwakilisha nchi katika mashindano ya klabu bingwa pamoja na Shirikisho.

Naamini kucheza na nyota kama Wayne Rooney, Ademola Lookman, Idrisa Gana, Gareth Barry, Aarone Lenon, Phil Jagielka, wachezaji wetu wangejifunza kitu kutoka kwa wakali hao wa kimataifa ambao wamepevuka kisoka tofauti na sisi.

Mbali na kujifunza kutoka kwa wakali hao lakini klabu zingeweza kujitangaza kimataifa pamoja na kuuza nyota wake nje ya mipaka ya Tanzania na kutimiza ndoto za vijana wa Kitanzania ambao wengi wao ndoto zao ni kucheza nje ya nchi.

Klabu zetu zimekuwa zikihaha kuuza nyota wake sehemu mbalimbali, lakini dili nyingi zimekuwa zikifa kutokana na wasifu kupitia Everton ilikuwa njia rahisi zaidi kwetu kuwauza nyota wetu kama Ibrahim Ajib, Kenny Ally, Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Atupele Green, Maka Mwakalukwa na wengine wengi, kwani wasaka vipaji wangeiangalia Tanzania kwa jicho la tatu.

Mawakala wengi kutoka pande mbalimbali za dunia wamekuwa wakipita mbali hadi Afrika Magharibi kwenda kutafuta vipaji vipya, lakini ukanda wetu tumekuwa tukisahaulika kila wakati, lakini nafasi pekee tulioambulia ni kuutangaza uwanja wa Taifa aibu iliyoje.

Viongozi wa klabu hizi hawapaswi kukwepa lawama katika hili kwani wao ndio walikuwa na uamuzi wa kuwabakiza wachezaji wa kikosi cha kwanza, inashangaza klabu kubwa inaleta kikosi cha vijana katika mashindano hayo ambayo timu za Kenya zilikuja kamili na hazikuja kupoteza hatimaye walivuna walichopanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles