24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga mawindoni VPL

Theresia Gasper-Dar es Salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa mechi nane kuchezwa katika viwanja tofauti, Simba wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, huku Yanga wakiwakaribisha Mbeya City, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba itashuka dimbani ikiwa imetoka kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Ijumaa iliyopita, huku Mtibwa Sugar wakiwa wamefungwa bao 1-0 na Lipuli FC, Dimba la CCM Gairo, Morogoro.

Yanga wao watakutana na Mbeya City wakiwa wametoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati Mbeya City wakitoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, Dimba la Jamhuri, Dodoma.

Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo, wakijikusanyia pointi 50 ndani ya mechi 20, wakati Mtibwa Sugar wapo nafasi ya 13 na pointi zao 23.

Yanga wao wanashika nafasi ya tatu wakijikusanyia pointi 37 kutokana na michezo 18, wakati Mbeya City wamejikita nafasi ya 18 na pointi zao 17.

Timu zote zitashuka dimbani zikiwa zinahitaji ushindi ili kuendeleza ushindani katika msimamo wa ligi na mwishowe kutwaa ubingwa.

Michezo mingine itakayopigwa leo, Azam FC watavaana na Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru, huku Singida United wakiikaribisha Namungo FC, Uwanja wa Liti, Singida.

Lipuli FC wataumana na JKT Tanzania, wakati Mwadui FC wakipepetana na Ndanda FC, huku Ruvu Shooting wakicheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Kagera Sugar ambao watawakaribisha Alliance, huku Biashara United wakikutana na Mbao FC, Uwanja wa Karume, Mara.

Akizungumzia mchezo wao, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema licha ya kuwa na kikosi kizuri, lakini wachezaji wake wanaonekana kuchoka kipindi cha pili na kushindwa kufanya kile wanachohitaji.

“Tunakutana na timu nzuri ambazo zimejiandaa vizuri, hivyo tutazidi kuwa makini kujituma na tusipoteze mchezo tena kwa mara nyingine katika mechi zinazotukabili mbele yetu,” alisema.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael, alisema anahitaji kupata ushindi katika mechi zao ili waendelee kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

“Ligi imeendelea kuwa na ushindani mkubwa hivyo tunahitaji kuzidisha ushindani kwa kufanya vizuri zaidi na kuwa makini, hasa eneo la umaliziaji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles