33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA marufuku Uwanja wa Taifa

dsc_7613*Serikali yazuia mapato

Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

SERIKALI imezipiga marufuku klabu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam pamoja na kuzuia mapato yaliyopatikana katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye uwanja huo.

Hatua hiyo imefikiwa na Serikali kufuatia vurugu zilizofanywa na baadhi ya mashabiki waliohudhuria mchezo huo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za uwanja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema Serikali imesikitishwa na kitendo hicho na kulazimika kuzifungia klabu hizo kucheza kwenye uwanja huo hadi itakapofanyika tathmini ya gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo.

“Tumesikitishwa sana na vitendo vilivyofanywa na mashabiki katika mchezo wa jana (juzi), kwani mbali na uvunjwaji wa viti pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na jingine upande wa Simba yamevunjwa.

“Kutokana na hali hiyo, tumelazimika kuzuia mapato yote ya mechi hadi tathmini itakapofanyika na kupata gharama za uharibifu uliotokea,” alisema.

Akielezea uharibifu huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo wa Wizara hiyo, Alex Nkenyenge, alisema mashabiki walivunja viti zaidi ya 1,781 na kuharibu mageti ya kuingia uwanjani hapo.

Alisema mapato yaliyopatikana katika mchezo huo ni zaidi ya Sh milioni 350, lakini klabu zote hazitapewa mgao ili kufidia uharibifu uliofanywa na gharama zikizidi huenda ikiwalazimu kuzilipia.

Aidha, akizungumzia malalamiko ya baadhi ya mashabiki waliodai mfumo mpya wa tiketi za kielektroniki kuacha kufanya kazi, Nkenyenge alisema mfumo huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na tatizo lililojitokeza lilitokana na mashabiki kuchelewa kufika uwanjani.

“Watu walichelewa kufika uwanjani, matokeo yake kila mmoja anataka kuingia kwa nguvu na kuanza kusukumana, wakati mfumo unataka kila mtu aingie kwa utaratibu,” alisema.

Wakati huo huo, klabu ya Simba imeomba radhi na kuelezea kusikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya mashabiki, huku ikikubali kulipia gharama za uharibifu huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, klabu hiyo imepanga kuzungumza na wamiliki wa Uwanja wa Taifa ili kujua namna ya kulipa gharama zinazotakiwa.

Pia Simba leo imepanga kuwasilisha malalamiko yake juu uchezeshaji mbovu wa waamuzi waliochezesha pambano la juzi na kuchangia kwa kiasi kikubwa mashabiki kufanya vitendo vya vurugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles