30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAITAMBIA YANGA

2

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema anajivunia kufunga mwaka huku timu hiyo ikiwa inaongoza katika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu inayoshirikisha jumla ya timu 16, baada ya juzi kuinyuka JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yaliiwezesha Simba kufikisha pointi 41, baada ya kushuka dimbani mara 17, wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, waliojikusanyia pointi 37, huku Kagera Sugar ikipanda hadi nafasi ya tatu kutokana na pointi 28 walizovuna.

Kutokana na uwiano wa pointi kwenye msimamo wa ligi, Yanga haiwezi kuishusha Simba kileleni hata ikishinda mchezo wao unaofuata dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, kwa kuwa tayari wanatofautiana kwa pointi nne.

Yanga imeshindwa kujiwekea mazingira mazuri ya kurejea kileleni mwa ligi hiyo baada ya kupoteza pointi muhimu dhidi ya African Lyon kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, Mayanja alisema wachezaji wanazidi kuimarika kadri michezo ya ligi inavyoendelea kuchezwa na kuonyesha matumaini ya kutimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa msimu huu, baada ya kuukosa kwa muda mrefu.

“Tunafurahishwa na matokeo mazuri tunayopata tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu, wachezaji wanaendelea kucheza kwa kujituma uwanjani na kuzidi kurahisisha kazi ya kunyakua ubingwa msimu huu,” alisema.

Aidha, kocha huyo raia wa Uganda aliwasifia wachezaji kwa kuonyesha soka safi la kuvutia, huku akielezea kufurahishwa na winga Pastory Athanas, aliyesajiliwa katika dirisha dogo akitokea klabu ya Stand United ya Shinyanga.

Winga huyo aliyesaidia kupatikana kwa bao  pekee la ushindi kwa Simba lililofungwa na Muzamiru Yassin, alionyesha uwezo mkubwa uwanjani, huku akiongoza kwa kuwasumbua mabeki wa JKT Ruvu.

Wekundu hao wa Msimbazi ambao wamepania kunyakua ubingwa wa msimu huu kutoka kwa mahasimu wao, Yanga, ambao wanaushikilia kwa misimu miwili mfululizo, waliboresha kikosi chao kwa kumsajili kipa Mghana, James Agyei, baada ya kufungwa mechi za mwisho kwenye mzunguko wa kwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles