29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

SIMBA YAIPAISHA TANZANIA AFRIKA

*Leo kuwashukia maafande wa Ruvu Shooting

WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

KITENDO cha Simba kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kimeifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi 12 zinazopewa nafasi nne kwenye mashindano ya Afrika.

Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya Jumamosi iliyopita kuichapa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mabao 2-1, mchezo wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hupima viwango vya nchi kupitia mafanikio ya vilabu vyake, kwenye mashindano ya Afrika kwa kipindi cha miaka mitano. Viwango vipya vitakavyotoka vikijumuisha mafanikio ya Simba 2018/19, vitaanzia 2015.

Kabla ya msimu huu, Tanzania ilikuwa nafasi ya 26 na pointi tatu zilizotokana na Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2016 na 2018.

Kutokana na kufuzu kwa Simba robo fainali msimu huu, kumeifanya Tanzania  kuwa na pointi 15 ambazo zikichanganywa na tatu za Yanga zimefika pointi 18.

Katika orodha hiyo, Morocco ndiyo inaongoza ikiwa na pointi 125.5, Tunisia 121.5, Misri 100.5, Algeria  89.5, DR Congo 82, Afrika Kusini 71.5, Zambia 35.5, Guinea, Nigeria na Sudan wana pointi 30 kila mmoja, Angola 21 na Tanzania 18.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Simba leo kinatarajia kushuka dimbani  kuvaana na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaorindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa wa 21 kwa Simba iliyopo nafasi ya tatu, katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 51, ikishinda 16, sare tatu na kupoteza mmoja.

Kikosi cha Simba chenye makao yake makuu Msimbazi jijini Dar es Salaam, jana kilifanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterani yakihusisha wachezaji 18 pekee.

Baadhi ya nyota wa Simba walikosekana kutokana na kupewa mapumziko, wengine wakijiunga na vikosi  vyao vya timu za Taifa ambazo zinajiandaa na michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika baadaye nchini Misri.

Wachezaji wa kimataifa walioondoka ni Meddie Kagere (Rwanda), Emmanuel Okwi, Jjuuko Murushid (Uganda) na Clatous Chama (Zambia).

Wekundu wa Msimbazi hao wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 5-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye uwanja huo.

Pia katika mchezo huo, Simba inatarajia kumtumia kipa namba mbili, Deogratius Munishi ‘Dida’, kutokana na Aishi Manula kuwa na majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Denis Kitambi, alisema wamejiandaa kuchukua pointi tatu na kupanda hatua nyingine katika msimamo wa ligi.

Alisema licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji, lakini waliopo wana uwezo wa kufanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi chao.

Kitambi alisema wamekuwa na nguvu zaidi ya kupigania pointi tatu kutokana na wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Yanga kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Lipuli FC kwa kufungwa bao 1-0.

“Tunaiheshimu Ruvu na tunajua mchezo wa soka hautabiriki, lakini malengo tuliyojiwekea ni kushinda mechi kesho (leo) na nyingine zilizobaki ili kutetea ubingwa wetu,” alisema Kitambi.

Kwa upande wake kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji, alisema amekiandaa vizuri kikosi chake ili kupambana na Simba.

Haji alisema anafahamu ubora wa Simba kwa sasa lakini hata yeye ana kikosi kizuri kutokana na matokeo aliyoyapata hivi karibuni.

“Simba wana wachezaji wazuri na sisi pia tuna kikosi bora, nashukuru wachezaji wote wapo katika hali nzuri, nina matumaini ya kuchukua pointi katika mchezo huo,” alisema kocha huyo.

Alitamba kuwa kikosi alichonacho sasa kina makali ya kutosha ukilinganisha na kilivyokuwa wakati wanaikabili Simba mzunguko wa kwanza, kutokana na usajili aliofanya dirisha dogo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Ruvu Shooting ipo nafasi ya 16 na pointi 35 baada ya kucheza mechi 30, imeshinda mechi nane, sare 11 na kufungwa 11.

@@@@@@@@@@@@@@

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles