31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yafunga mitaa Dar

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MAMIA ya mashabiki wa soka wa klabu ya Simba jana walijitokeza kuipokea timu yao hiyo ilipokuwa ikitoka Morogoro ambako ilikabidhiwa rasmi  kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018-19.

Makabidhiano ya kombe hilo  yalifanyika mara baada ya mchezo kati ya timu hiyo na Mtibwa Sugar, uliochezwa Uwanja wa Jamhuri na kumalizika kwa  suluhu.

Hiyo ni mara ya pili kwa Wekundu hao kubeba taji hilo baada ya kufanya hivyo pia msimu wa 2017-18.

Simba ilitetea ubingwa wake wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 93 katika mechi 38 ilizocheza, ikishinda michezo 29, sare sita na kupoteza mechi tatu.

Msafara wa timu ya Simba uliingia viunga vya Jiji la  Dar es Salaam saa sita mchana na kulakiwa na mashabiki wengi wa timu hiyo ambao  walikuwa  wamejikusanya katika matawi mbalimbali ya klabu yao.

Wachezaji wa timu hiyo walikuwa wamekaa kwenye gari la wazi, huku wakiwa wamebeba kombe lao wakishangilia na kuwapungia mikono mashabiki wao.

Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walikuwa wakiendesha bodaboda, bajaji na  magari kwa  mbwembwe wakionyesha furaha yao, huku wengine wakitembea kwa miguu na kuimba nyimbo za kujitapa.

amshaamsha hiyo iliendelea hadi pale msafara wa timu hiyo ulipowasili Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyoko Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles