Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
MAMIA ya mashabiki wa soka wa klabu ya Simba jana walijitokeza kuipokea timu yao hiyo ilipokuwa ikitoka Morogoro ambako ilikabidhiwa rasmi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018-19.
Makabidhiano ya kombe hilo yalifanyika mara baada ya mchezo kati ya timu hiyo na Mtibwa Sugar, uliochezwa Uwanja wa Jamhuri na kumalizika kwa suluhu.
Hiyo ni mara ya pili kwa Wekundu hao kubeba taji hilo baada ya kufanya hivyo pia msimu wa 2017-18.
Simba ilitetea ubingwa wake wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 93 katika mechi 38 ilizocheza, ikishinda michezo 29, sare sita na kupoteza mechi tatu.
Msafara wa timu ya Simba uliingia viunga vya Jiji la Dar es Salaam saa sita mchana na kulakiwa na mashabiki wengi wa timu hiyo ambao walikuwa wamejikusanya katika matawi mbalimbali ya klabu yao.
Wachezaji wa timu hiyo walikuwa wamekaa kwenye gari la wazi, huku wakiwa wamebeba kombe lao wakishangilia na kuwapungia mikono mashabiki wao.
Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walikuwa wakiendesha bodaboda, bajaji na magari kwa mbwembwe wakionyesha furaha yao, huku wengine wakitembea kwa miguu na kuimba nyimbo za kujitapa.
amshaamsha hiyo iliendelea hadi pale msafara wa timu hiyo ulipowasili Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyoko Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.