Simba yafanya ‘mauaji’

0
400

 MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM 

TIMU ya Simba jana iliishushia kipigo kikali cha mabao 5-1 Alliance,katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Mabao ya Wekundu hao wa Msimbazi yaliwekwa wavuni na Meddie Kagere, aliyefunga mawili dakika ya 23 na 44, mengine yakifungwa na Luis Miquissone dakika ya 64, Deo Kanda dakika ya 75 na Said Ndemla dakika ya 86. 

Bao la kufutia machozi la Alliance lilifungwa na Martin Kigi dakika ya 38. 

Ushindi huo unakuwa wa kwanza kwa Simba, tangu ilipotwaa taji la Ligi Kuu msimu huu Juni 29, mwaka huu, baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prison, Uwanja wa Sokoine, Mbeya. 

Simba kwa ushindi huo imefikisha pointi 84, baada ya kucheza michezo 36, ikishinda 26, sare sita na kupoteza minne. 

Kipigo hicho kinazidi kuiweka Alliance katika mazingira hatarishi ua kushuka daraja,ikishika nafasi 17 na pointi 41, baada ya kucheza michezo 36 , ikishinda 10, sare 11 na kupoteza 15. 

Vijana hao wa kocha Kessy Mziray wanatakiwa kushinda michezo yao miwili iliyobaki ili kukusanya pointi sita zitakazo fufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu msimu ujao. 

Mchezo huo ulianza kwa kasi, simba ikionekana kujiamini zaidi na kutawala eneo la kiungo. 

Alliance ilionekana kuingia na tahadhari, ikitumia pasi ndefu kulifikia langoni la Simba. 

Dakika ya tisa, Kigi alishindwa kuitumia vema nafasi aliyopata kuindikia Alliance bao la kuongoza, baada ya kupokea pasi nzuri ya Juma Nyangi na kuachia shuti lililokwenda nje ya lango. 

 Dakika ya 22, Mlinda mlango wa Alliance, John Mwanda alimwangusha Miquissone ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuipa Simba penalti.

Dakika 23, Kagere aliindikia Simba bao kuongoza kwa mkwaju wa penati, hata hivyo dakika moja badae alilimwa kadi ya njano kwa kosa la kuonyesha fulana ya ndani wakati akishangilia bao lake.

Dakika ya 30, nahodha wa Alliance, Israel Patrick alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa hatari uliotokana na shuti la Miquissone.

Dakika ya 38, Kigi aliisawazishia Alliance bao, akimalizia kazi nzuri ya Michael Chinedu, aliyepora mpira kwa kiungo Jonas Mkude kisha kuwalamba chenga mabeki wa Simba kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Dakika ya 44, Kagere aliifungia Simba bao la pili, baada ya kumegewa pande safi na Francis Kahata.Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, kipindi cha pili, Kocha wa Simba Sven Vanden Bloeck alifanya mabadiliko, alimtoa Mkude na nafasi yake kuchukuliwa na Mzamiru Yassin.

Dakika ya 57, Sameer Vicent alilimwa kadi ya njano, baada ya kumchezea rafu Mzamiru.

Dakika ya 64, Miquissone aliifungia Simba bao la tatu kwa shuti kali lililomshinda Mwanda.

Dakika ya 67, Simba ilifanya mabadiliko, alitoka Francis Kahata na nafasi yake kuchukuliwa na Deo Kanda.

 Dakika ya 73, Shabani William wa Alliance alilimwa kadi ya njano, baada ya kumchezea rafu Shomari Kapombe.

Dakika ya 75, Kanda aliifungia Simba bao la nne, akimalizia krosi ya Kagere.

Dakika ya 78, Simba ilifanya mabadiliko mengine, alitoka Miquissone na Clatous Chama na nafasi zao kuchukuliwa na Ndemla na Hassan Dilunga kabla ya Kigi kutoka kwa upande wa Alliance na kuingia Zabona Hamis. Dakika ya 86, Ndemla aliindikia Simba bao la tano kwa shuti kali akimalizia vema pasi ya Dilunga.

Dakika 90 za mchezo huo zilikamilika kwa Simba kuondoka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Alliance.

Mbali na mchezo huo, ligi hiyo iliendelea katika viwanja vingine viwili, Azam ilishindwa kutamba ugenini baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Mbao iliilazimisha sare ya bao 1-1 JKT Tanzania, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here