NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM
KIKOSI cha timu ya soka ya Simba kiliondoka jana kuelekea mkoani Morogoro kujichimbia katika kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Simba inaanza maandalizi rasmi huku ikiwa imepania kurejesha hadhi yake msimu ujao chini ya Kocha Mkuu mpya Mcameroon, Joseph Omog pamoja na msaidizi wake, Mganda Jackson Mayanja aliyefundisha msimu uliopita.
Kikosi cha wachezaji 31 kinachojumuisha nyota wapya waliosajiliwa kwa msimu ujao na wale waliong’ara msimu uliopita, wameitwa kwenye kambi hiyo ambayo itadumu hadi mwezi ujao ambapo pia kitacheza mechi za kirafiki.
Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, aliliambia MTANZANIA jana kuwa timu imeondoka ikiwa na nia thabiti ya kurejesha heshima ya Simba, huku akidai kambi ya sasa itakuwa tofauti kabisa na zile walizoweka msimu uliopita.
“Timu imeondoka saa 7:00 mchana leo (jana), tunashukuru mipango yetu imekwenda kama tulivyopanga ikiwemo wachezaji kuwasili kwa wakati huku wakiwa na morali ya hali ya juu, hivyo napenda kuwaambia mashabiki wasiwe na wasiwasi mambo yapo safi,” alisema Aveva.
Alisema kikosi hicho kitajichimbia katika Hosteli za Kanisa la Baptist zilizopo Milima ya Uluguru kwani ni sehemu nzuri ambayo mandhari yake inaendana na hadhi ya klabu ya Simba.
Aidha, Aveva alithibitisha kuwa kiungo mpya, Shizza Kichuya, aliyetua Simba akitokea timu ya Mtibwa Sugar ni miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye kambi hiyo.
Aliwataja wachezaji walioingia kambini kuwa ni Nahodha Mussa Hassan ‘Mgosi’, Vincent Angban, Awadhi Juma, Said Ndemla, Peter Mwalyanzi, Peter Manyika, Dennis Richard, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hajji Ugando, Novatus Lufunga, Mwinyi Kazimoto, Daniel Lyanga na Ibrahim Ajib.
Wapya walioripoti hadi kufikia jana ni Mohammed Kijiko, Moses Chibandu, Said Mussa, Muzamir Yassin, Mohammed Ibrahim, Frederick Blagnon, Kelvin Falu, Vincent Costa, Method Mwanjali, Janvier Besala Bokungu na Mussa Ndusha.