SIMBA YABANWA MTWARA

0
1593

Na MWANDISHI WETU, MTWARAMabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba, imelazimishwa suluhu na wenyeji wao, Ndanda FC, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara jana.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi saba baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda miwili na kulazimishwa sare mmoja.

Timu hiyo ilianza ligi kwa kuichapa Tanzania Prisons bao 1-0, kisha ikailaza Mbeya City mabao 2-0, kabla ya jana kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji wao, Ndanda.

Ndanda sasa imefikisha pointi nne baada ya kucheza michezo minne, ikishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza miwili.

Mchezo huo ulianza kwa kasi. Simba ilikuja juu na kumiliki mpira na kutengeneza nafasi kwa ajili ya kuhakikisha inapata bao la mapema.

Katika dakika ya nne, Mohamed Hussein alishindwa kuiandikia Simba bao la kuongoza baada ya kupokea pasi ya kichwa kutoka kwa Emmanuel Okwi na kuachia shuti lililopita juu ya lango la Ndanda.

Katika dakika ya 15, Okwi alipoteza nafasi nyingine akiwa katika eneo zuri, baada ya kupokea krosi ya Shomari Kapombe na kuachia mkwaju uliokwenda nje kidogo ya lango la Ndanda.

Simba iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao. Katika dakika ya 16, Meddie Kagere alishindwa kuiandikia Simba bao la kuongoza baada ya kupokea pasi ndefu ya Mohamed Ibrahim na kupiga kichwa na mpira kutoka nje.

Katika dakika ya 34, John Bocco alipoteza nafasi ya kuipatia timu yake bao, baada ya kushindwa kumalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mohamed Hussein.

Katika dakika ya 39, Bocco alishindwa kutumia vema makosa ya mabeki ya Ndanda waliojichanganya na kushindwa kuondoa mpira wa hatari langoni mwao, Bocco aliachia shuti lililokwenda nje.

Kipindi cha kwanza kilimalizika wa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana, licha ya Simba kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi ambazo walishindwa kuzitumia.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa wenyeji Ndanda kuzinduka na kufanya mashambulizi kadha langoni mwa Simba.

Katika dakika ya 46, Aishi Manula alisimama imara na kuokoa mchomo hatari uliopigwa na Vitalis Mayanga, ambaye aliachia mkwaju akiwa nje ya 18 ya Simba.

Katika dakika ya 56, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kumtoa Mohamed Ibrahimu na kumwingiza Clotus Chama.

Katika dakika ya 58, Mwamuzi Nassoro Mwinchui alimlima kadi ya njano Hassan Nassoro wa Ndanda, baada ya kumchezea rafu Jonas Mkude.

Katika dakika ya 59, Simba ilifanya mabadiliko mengine. Alitoka Emmanuel Okwi aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na James Kotei.

Katika dakika ya 74, ilifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Kagere na kuingia Adam Salamba.

Katika dakika ya 88, kocha wa Ndanda, Malale Hamsini alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake, alimtoa Hassan Nassoro na kumwingiza Moshi Salumu.

Licha ya mabadiliko hayo, hadi dakika tisini zinamalizika, timu hizo zilitoka uwanjani bila kufungana.

Ligi hiyo iliendelea katika viwanja vingine vitano, ambako Lipuli ikiwa nyumbani ilijikuta ikilazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar katika mchezo uliochezwa Uwanja Samora, Iringa.

Mbao FC ilishindwa kutamba nyumbani baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Tanzania katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Maafande wa Jeshi la Magereza nchini, Tanzania Prisons, walishindwa kuondoka na pointi tatu nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Ruvu Shooting.

Singida United ikiwa ugenini ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao, KMC, katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Biashara United ikiwa nyumbani ilishindwa kuvuna pointi tatu baada ya kulazimishwa suluhu na Kagera Sugar katika mchezo uliochezwa katika Uwanja Karume, mkoani Mara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here