21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

SIMBA YABADILISHIWA MWAMUZI GHAFLA

  • Ni wa mchezo wao wa marudiano na TP Mazembe Lubumbashi
  • Muethiopia apokonywa rungu na kukabidhiwa Mzambia, Msimbazi waigomea Caf

SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limefanya mabadiliko ya waamuzi watakaochezesha mechi ya marudiano ya robo fainali kati ya Simba na TP Mazembe itakayopigwa Jumamosi Uwanja wa Mazembe, Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Taarifa iliyotolewa na Caf jana imeeleza kuwa mwamuzi wa kati wa mchezo huo sasa atakuwa Janny Sikazwe wa Zambia badala ya Bamlak Tessema wa Ethiopia.

Kwa mujibu wa Caf, mwamuzi msaidizi namba moja atakuwa, Berhe Tesfagiorgis O’Michael wa Eritrea, wakati mwamuzi msaidizi namba mbili atakuwa Romeo Kasengele wa Zambia.

Kabla ya mabadiliko hayo, mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Tesmegin Atango wa Ethiopia na Gilbert  Kipkoech ambaye alipangwa kuwa mwamuzi msaidizi namba mbili.

Kwa upande wa mwamuzi wa akiba, baada ya mabadiliko hayo sasa atakuwa Audrick Nkole wa Zambia badala ya Peter Waweru wa Kenya.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayajamgusa kamisaa wa mchezo huo ambaye ataendelea kuwa Aimable Habimana wa Burundi.

Kwa mujibu wa Caf, uamuzi huo umefanyika kutokana na sababu za kiufundi ambazo hazikuwekwa wazi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Creacentius Magori, alikiri klabu yao kupokea taarifa ya Caf jana asubuhi ikiwaeleza juu ya mabadiliko hayo na kusema kuwa tayari wameliandikia barua ya malalamiko shirikisho wakihoji sababu za kufanyika uamuzi huo.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya malalamiko ya Simba iliyosainiwa na Magori na ambayo MTANZANIA lilifanikiwa kuiona, Wekundu hao wamedai kushangazwa na mabadiliko hayo kufanywa bila sababu zilizoshawishi kuwekwa wazi.

Iliendelea kueleza kuwa uamuzi huo wa Caf utasababisha kuwapo kwa minong’ono  ya klabu yao kutotendewa haki wakati wa mchezo huo, kwa kuzingatia nchi ya Zambia anakotoka mwamuzi mpya na DRC ambako ni maskani ya TP Mazembe, zina uhusiano wa karibu.

Kwa mantiki hiyo, klabu ya Simba iliitaka Caf kubatilisha uamuzi huo na kuwarejesha waamuzi wa awali kama njia itakayoondoa mashaka.

Pambano la kwanza kati ya Simba na Mazembe lilifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa suhulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,717FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles