26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

SIMBA YA WAADHIBU MAAFANDE WA APR

NA THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM


TIMU ya Simba SC, imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la  Kagame’, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu inayomilikiwa na Jeshi la Rwanda ya APR, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Adam Salamba dakika ya 73 na Meddie Kagere dakika ya 90.

Kwa ushindi huo, Simba ilifikisha pointi sita na kujikita katika uongozi wa msimamo wa kundi C.

APR walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Simba dakika ya 22, lakini kiki ya Imanishimwe Emmanuel, ilipanguliwa na kipa wa Simba, Ally Salim.

Simba ilijibu kwa kufanya shambulio dakika ya 24, lakini Ally Shomari, alishindwa kuunganisha wavuni mpira wa krosi iliyochongwa na Marcel Kaheza.

Kosa kosa ziliendelea kila upande hadi pale dakika 45 za kipindi cha kwanza zilipomalizika pasipo nyavu kutikisika.

Kipindi cha pili, kila timu iliongeza kasi ya mashambulizi, dakika ya 59, kipa wa Simba, Salim, alifanya kazi ya ziada baada ya kupangua shuti la Dominique Savio.

Mashambulizi ya APR, yalizaa matunda dakika ya 68 baada ya mshambuliaji, Nkinzingabo Fiston, kuifungia timu hiyo bao la kuongoza baada ya mkwaju wake kumshinda kipa wa Simba, Ally Salim na kujaa wavuni.

Bao hilo ni kama liliiamsha Simba ambayo ilifanikiwa kusawazisha dakika ya 73 kupitia kwa Salamba aliyeunganisha mpira uliopigwa na Marcel Kaheza.

Baada ya kusawazisha bao hilo, Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 73, alitoka Kaheza na kuingia Mohammed Rashid kabla ya dakika ya 74 kutoka Ally Shomary na nafasi yake kuzibwa na Nicholas Gyan.

Mabadiliko hayo yaliiongezea nguvu Simba na kufanikiwa kuandika bao la pili na la ushindi dakika ya 90 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Kagere ambaye huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza tangu alipojiunga na Wekundu hao akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Mwamuzi wa mchezo huo, Ssali Mashood, aliamuru ipigwe penalti hiyo baada ya beki wa APR, Nsabimana Aimable, kumfanyia madhambi Kagere ndani ya eneo ya hatari.

Katika mchezo mwingine wa kundi C uliopigwa mchana, Singida United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dakadaha ya Somalia. Bao pekee la Singida lilikwamishwa wavuni na Habibu Kiyombo dakika ya 54.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,621FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles