27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA WANAMUOKOA MSICHANA WA MIAKA 12

*Wamlinda saa 12 dhidi ya wanaume wabakaji


NI tukio la ajabu na kweli lililotokea mwaka 2005 nchini Ethiopia wakati binti wa miaka 12 alipookolewa na simba wakubwa watatu dhidi ya wanaume saba waliokuwa wamemteka.

Wanaume hao walimteka na kumpa vipigo binti huyo mdogo katika jaribio la kumlazimisha aolewe na mmoja wao.

Bahati mbaya kwao na nzuri kwa msichana huyo japo kwa namna ya kutisha, wanaume waliweka maficho porini pakiwa mahala pasipo sahihi na wakati usio sahihi.

Wakati msichana akilia kuomba msaada, simba wakubwa watatu walijitokeza kutoka kusikojulikana wakiwa na hasira wakawatimua wanaume hao kutopka eneo hilo. Kisha simba hao wakamwendea msichana na kumlinda kwa muda wa saa 12.

Kwa mujibu wa polisi, simba walisimama na kumlinda binti huyo hadi polisi na maofisa wengine waliokuwa wakimtafuta walipojitokeza mahali walipo.

Simba walimuacha mtoto huyo salama salimini bila kumdhuru popote na kutokomea porini.

Tukio la msichana huyo aliyetoweka kwa wiki moja lilitokea katika mji wa Bita Genet, uliopo karibu maili 350 kusini magharibi mwa Addis Ababa.

“Walisimama muda wote wakimlinda na walipotuona, walimuacha kama zawadi na kutokomea msituni,” Sajenti Wondimu Wedajo alikaririwa akisema kipindi hicho.

“Iwapo simba wasingejitokeza kumuokoa, ingekuwa hatari zaidi, kwa maana mara nyingi mabinti wadogo kama hao hupigwa na kubakwa kwa lengo la kulazimishwa kuolewa,” alisema.

Naye Tilahun Kassa, ofisa wa serikali ya mtaa alikubaliana na kilichoelezwa na Sejenti Wondimu akisema mmoja wa wanaume alitaka kumuoa msichana kinyume na matakwa yake.

“Kila mtu anadhani hii ni aina fulani ya miujiza, kwa sababu kwa kawaida simba hushambulia watu,” Wondimu alisema.

Mtaalamu wa Wanyamapori, Wizara ya Maendeleo Vijijini,  Stuart Williams alisema huenda msichana alinusurika na simba hao kwa sababu ya kilio cha kuogofya alicholia kutokana na shambulio la wanaume hao.

“Kilio cha msichana mdogo huenda kilidhaniwa kuwa cha simba mtoto, kitu ambacho kinaeleza kwanini hawakujihangaisha kumla,” Williams alieleza.

Simba wa Ethiopia wanaofahamika kwa manyoya yao makubwa meusi, ni alama ya taifa na nembo zinazohusudiwa na taswira zao zipo kwenye sarafu ya nchi hiyo.

Pamoja na kampeni ya karibuni dhidi ya majangili, wahalifu huwinda ngozi yao, ambayo huweza kugharimu dola 1,000 sawa na Sh milioni 2.2.

Williams anakadiria kwamba ni simba 1,000 tu wa Ethiopia waliobakia msituni.

Msichana huyo alioweza kutibiwa kwa majeraha na watekaji wanne kati ya saba walikamatwa mara moja.

Utekaji wasichana hao kwa muda mrefu ulikuwa sehemu ya utamaduni wa Ethiopia.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wasichana nchini Ethiopia hutekwa, vitendo vinavyotokea zaidi maeneo ya vijijini ambako ndiko iliko sehemu kubwa ya wakazi milioni 71 wa taifa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles