24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Simba waapa kupindua meza

NA MOHAMED KASARA-DAR ES SALAAM


KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi, Simba, leo kitakuwa na kibarua kizito cha kusaka pointi tatu dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba inakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 20, nyuma ya Yanga, iliyoko nafasi ya pili na pointi 22 na Azam inayokamata uongozi wa ligi ikiwa na pointi 24.

Vigogo hao wa Msimbazi wamejikita katika hatua hiyo, baada ya kucheza michezo tisa, ikishinda sita, sare mbili na kupoteza mmoja.

Wekundu hao watashuka dimbani mara hii wakitoka kuichapa Alliance FC mabao 5-1 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo.

Ruvu Shooting inayokutana na Simba, inashika nafasi ya 12, ikiwa na pointi 13, baada ya kucheza michezo 10, ikishinda mitatu, sare nne na kupoteza mitatu.

Wanajeshi hao wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wataingia uwanjani wakiwa na morali ya juu iliyotokana na ushindi wao wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Singida United katika mchezo uliopita wakiwa nyumbani Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Lakini maafande hao wanaweza kuingiwa na mchecheto kama wataangalia rekodi yao ya msimu uliopita, ambao walipoteza pointi zote sita katika michezo miwili ya ligi hiyo.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Agosti 26 mwaka jana, Simba iliishushia Shooting kipigo cha mabao 7-0, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili, Februari 4 mwaka huu, michezo yote ikipigwa  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji wao wamekubaliana kuhakikisha wanashinda kila mchezo ili kupata pointi nyingi zitakazowawezesha kutetea ubingwa walioutwaa msimu uliopita.

Katika kuhakikisha hilo linatimia, Aussems amemtaka mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi, kuacha ubinafsi wa kutaka kufunga hata katika mazingira magumu, badala yake awe mwepesi wa  kugawa pasi kwa wachezaji wenzake walioko katika nafasi nzuri zaidi.

“Wachezaji wangu wote nimewafundisha mbinu za kufunga,
mabao tunayopata ni machache, tofauti na nafasi ambazo tunatengeneza,  nimemwambia Okwi aache tabia ya uchoyo na kulazimisha kufunga hata sehemu ambayo amebanwa, na wenzake wapo katika nafasi nzuri.

“Tunataka kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili kuvuna pointi za kutosha kutetea ubingwa wetu, ni muhimu kujua kuwa wachezaji wanapokuwa uwanjani  wanahitaji ushirikiano ambao utaisaidia timu kushinda mchezo,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao, Ruvu Shooting, Ofisa Habari wa Shooting, Masau Bwire, alitamba kuwa kikosi chao kinawamudu vilivyo wapinzani wa Simba ambao watapambana nao katika mchezo huo utakaoanza  saa 1:00 usiku.

“Kikosi chetu kipo ngangari kwa ajili ya kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo huo, baada ya kufanikiwa kuilaza Singida mabao 3-0, nguvu zetu zote tumezielekeza katika mchezo dhidi ya Simba, wasitarajie watatupiga kizembe kama msimu uliopita, safari hii tunakuja kivingine, wajiandae kisaikolojia kupokea kichapo,” alisema Bwire.

Patashika nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya JKT Tanzania dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo utakaoanza majira saa 8:00 mchana katika Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo, Dar es Salaam.

Vinara wa ligi hiyo, Azam FC wataumana na Singida United, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Namfua, Manispaa ya Singida.

Vibonde wa ligi hiyo, Alliance FC, watakuwa na shughuli pevu ya kuhakikisha wanabakiza pointi tatu nyumbani mbele ya Coastal Union, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Nao Wakata miwa, Mtibwa Sugar watakabiliana na ndugu zao, Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles