25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

SIMBA Vs YANGA LEO Dakika 90 kumaliza tambo

NA ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM

DAKIKA 90 zitamaliza tambo za watani wa jadi, timu ya Simba na Yanga, ambazo leo zitashuka dimbani kuumana, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mgeni rasmi wa mchezo huo unaofahamika pia kwa lugha ya kigeni ‘Kariakoo Derby’ mchezo wa timu pinzani zinazotokea katika mji mmoja ni Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad , aliyewasili jana hapa nchini.

Timu hizo zitaingia dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2, katika mchezo wa mzunguko wa kwanzam, uliochezwa Januari 4, mwaka huu kwenye uwanja huo.

Simba itaikabili Yanga, ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikikusanya pointi 68, ilizovuna baada ya kucheza michezo 26, ikishinda 22, sare mbili na kupoteza miwili.

Yanga ipo nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 47, baada ya kucheza mechi 24, ikishinda 13, sare nane na kupoteza mitatu.

 Simba itaingia dimbani ikitoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam,  mchezo uliochezwa katikati ya wiki iliyopita kwenye uwanja huo.

Yanga nayo, itaingia uwanjani ikiwa na morali ya juu, baada ya kuichakaza Mbao mabao 2-0, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa.

Mara ya mwisho timu hizo kuumana tarehe kama ya leo ilikuwa Machi 8 msimu wa 2014/15, ambapo Simba ilishinda bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji Emannuel Okwi, dakika ya 52.

Mchezo wa leo utakuwa wa ushindani mkubwa, kutokana na sababu tatu, Simba kutaka kuvuna pointi tatu ili kufupisha safari ya kusaka ubingwa, Yanga kutaka ushindi ili kuzidi kuibana Simba na upinzani wa kihistoria wa timu hizo.

Timu hizo zilipokutana msimu uliopita, matokeo yalikuwa suluhu mzunguko wa kwanza kabla ya Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya Yanga mzunguko wa pili.

Yanga inajivunia maboresho ya kikosi yaliyofanyika dirisha dogo, hasa usajili wa kiungi mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison, ambaye ameibuka kuwa kipenzi cha Wanajangwani.

Pia uwapo wa kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyerejea kikosini hapo dirisha dogo.

Niyonzima aliichezea Yanga kwa miaka sita na kuipa mataji mengi kabla ya kutimkia Simba na kisha timu ya kwao ya AS Kigali.

Wakali wengine wa Yanga ni Papy Tshishimbi, Lamine Moro, Patrick Sibomana, Kelvin Yondani, Juma Abdul, Ditram Nchimbi, Mapinduzi Balama, Feisal Salum,  Adeyum Saleh, Mohamed Issa na Ally Sonso.

Kwa upande mwingine, Simba itawategemea  Luis  Miquissone, John Bocco, Meddie Kagere na Clatous Chama.

Lakini jicho la kipekee litaelekezwa kwa  Luis, mkali wa kucheza na nyavu aliyetua Msimbazi dirisha dogo akitokea US Songo ya Msumbiji.

Wakizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, makocha wa timu hizo kila mmoja ametamba kupata ushindi.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema licha ya kwamba hiyo itakuwa mara yake ya kwanza kuwapo katika benchi la timu hiyo ikiivaa Simba, anaamini kimeiva kwa vita hiyo ya kusaka pointi tatu.

“Najua ni mechi ya derby, kila timu imejiandaa kushinda, kwangu nahitaji alama tatu za mchezo huo na wapinzani wangu wanahitaji alama tatu muhimu za mchezo huo, nina amini mchezo utakuwa mzuri na kila timu itapambana kuhitaji matokeo mazuri”alisema Eymael.

Nahodha wa Yanga, Juma Abdul alisema wataingia uwanjani  kuwakabili wapinzani wao wakifuata maelekezo ya kocha wao ili kupata ushindi.

Naye kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema  anatarajia kikosi chake kucheza vizuri na kupata matokeo ya ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Alisema upande wao  kila mmoja yupo fiti isipokuwa kwa Miraji Atumani na Said Ndemla  ambao ni majeruhi.

 “Tumejiandaa kushinda tunahitaji pointi tatu muhimu za mchezo huo, maandalizi kwa kila mchezaji mmoja mmoja yapo vizuri, nina amini tutapata tunachotarajia dhidi ya wapinzani wetu.

Nahodha wa Simba, Bocco, alisema wao wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa kesho, wanaenda kucheza ili wapate pointi tatu muhimu za mchezo huo .

“Sisi kama wachezaji tumejiadaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu na Yanga, Tunaahidi kwenda kucheza mchezo wa kujituma ili tuwafurahishe mashabiki wetu na ili tuweze kupata alama zote tatu za mchezo huo” alisema Boccco.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles