Na WINFRIDA MTOI- DAR ES SALAAM
LIGI Kuu Tanzania Bara, inatarajia kuendelea leo kwa michezo miwili, itakayopigwa jijini Dar es Salaam, Simba ikiikabili Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, wakati Azam FC itaumana na Mbao dimba la Azam Complex.
Timu hizo zinarejea dimbani ikiwa ni zaidi ya miezi miwili, tangu ligi hiyo ilivyosimama kutokana na janga la corona.
Simba ikiwa ni bingwa mtetezi wa ligi hiyo, inaongoza katika msimamo ikiwa na pointi 71, huku Ruvu Shooting ikishika nafasi ya 11 na alama 39, zote zikicheza michezo 28.
Nayo Azam, ipo nafasi ya pili na pointi 54, wakati Mbao ikiburuza ikiwa katika nafasi ya 19 na pointi 22, zote zikishuka dimbani mara 28.
Michezo hiyo ni muhimu kwa timu zote, kila moja itapigania pointi tatu kwa lengo la kutaka kufikia malengo iliyojiwekea ligi itakapofikia ukomo.
Simba tayari ilishaweka wazi kuwa,inahitaji pointi 12 katika michezo minne, ili kutawazwa mabingwa wa msimu huu.
Kwa kuzingatia hilo, leo Wekundu hao watahakikisha wanaanza safari yao vizuri kwa kupata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting.
Mchezo kati ya timu hizo, unatarajiwa kuwa wa vuta nikuvute, kwani Ruvu Shooting nayo itataka kulipa kisasi sambamba na kumaliza uteja wake kwa Simba.
Lakini pia, ushindi ni muhimu kwa Ruvu Shooting kwavile nayo haiko mbali sana na mstari hatari wa kushuka.
Kwa misimu mitatu mfululizo timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), wameshindwa kuvuna pointi yote walipokutana na Simba.
Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 23 mwaka jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Simba ilishinda mabao 3-0.
Msimu wa 2018/2019, Simba ilishinda mabao 5-0 mzunguko wa kwanza kabla ya kushinda mabao 2-0 mzunguko wa pili.
Msimu wa 2017/18, Simba ilishinda mabao 7-0 mzunguko wa kwanza Uwanja wa Uhuru kabla ya kutakata mabao 3-0 mzunguko wa pili Uwanja wa Uhuru.
Simba inajivunia rekodi nzuri za kuondoka na matokeo ya ushindi mbele ya Ruvu, lakini leo itakuwa na kibarua kigumu kutokana na sababu nilizokwisha zitaja.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema anatarajia utakuwa mgumu lakini ameridhika na viwango vya wachezaji wake, anaamini atafanya vizuri katika mechi zote zilizobaki.
Sven alisema, akiwa mazoezini siku zote amekuwa akiweka msisitizo katika mbinu na stamina kwa kila mchezaji.
“Morali ya wachezaji iko juu na wanajitahidi kufuata maelekezo ninayowapa, nina matumaini ya kufanya vizuri kwa kuanzia mchezo wa Jumapili,” alisema Sven.
Naye Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema wamejipanga vilivyo kwani Simba kipindi hiki isitegemee mteremko wa kujichukulia pointi.
“Kocha Mkuu wa timu Ruvu Shooting, Salum Mayanga, anamekamilisha program yake, vijana wameiva kisawasawa, tupo tayari kuwaonesha Simba soka la kiwango cha juu,” alisema Bwire.
Kwa upande wa Azam inakutana na Mbao ikiwa imetoka kuifunga timu hiyo bao 1-0 katika mechi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mchezo wa leo kati ya Azam na Mbao, unatarajia kushudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, DkHassan Abbas, akiwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Thabit Zakaria, alisema Dk Abbas, atakuwa mgeni rasmi kwakua mchezo huo utachezwa sambamba na tukio la uchangiaji wa damu.
sssssssssssssssssssssssssssssssss
Mabondia maveteran mbioni kupata mtetezi
Na VICTORIA GODFREY-DAR ES SALAAM
MABONDIA wa zamani wa ngumi nchini, wapo mbioni kukamilisha mchakato wa kuanzisha chama chao kitakachoshirikisha maveterani wa ngumi wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini hapa , Katibu wa Muda wa kikundi hicho, George Andrew, alisema lengo ni kuhakikisha wanashirikiana na kusaidiana nyakati za shida na raha.
Alisema tayari wamefanya vikao na kuandaa katiba ya chama chao na sasa wanatarajia kukutana Juni 28 mwaka huu ili kupanga tarehe ya kuiwasilisha kwa msajili.
“Muungano huu umekuja baada ya kuguswa na wenzetu ambao sasa ni wagonjwa ambao ni Antony Mwang’onda na Willy Isangura, huu utahusu mabondia wote wa zamani, lengo ni kushirikiana na kudumisha upendo na amani miongoni mwetu,”alisema Andrew.
Andrew alisema walengwa wa chama hicho ni watu wote walioshiriki mchezo wa ngumi, wakiwamo mabondia waliocheza kuanzia ngazi ya shule, klabu na taifa, waamuzi ,viongozi na makocha.