26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Polisi Tanzania hapatoshi leo

Theresia Gasper – Dar es Salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo huku vinara wa Ligi hiyo Simba SC wakishuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuwakaribisha Polisi Tanzania.

Simba wanakutana na Polisi Tanzania wakiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union mwishoni mwa wiki iliopita.

Upande wao Polisi Tanzania wao wanakutana na Simba wakiwa wametoka kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Simba inaongoza katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 47 baada ya kucheza michezo18, wakishinda michezo 15 na kutoka sare michezo miwili huku wakifungwa mchezo mmoja.

Wakati huo Polisi Tanzania wapo nafasi ya saba wakiwa na pointi 30, sawa na Coastal Union pamoja na Kagera Sugar wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba wataivaa Polisi Tanzania wakiwa wanahitaji kuendeleza ushindi ili kujikita kileleni katika msimamo wa ligi pamoja na kutetea ubingwa wao.

Pia huo utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana tangu Polisi Tanzania ifanikiwa kupanda ligi kuu msimu huu.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven VandenBroeck, alisema mipango yake ni kuendeleza ushindi na kutoruhusu kufungwa bao hata moja.

“Nahitaji kila mchezaji afahamu majukumu yake uwanjani ili aweze kufanya vizuri kwani usipokuwa makini unaweza ukapoteza mchezo kirahisi,” alisema.

Upande wake Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Hamsini Malale, alisema wamejiandaa kiushindani ukizingatia wanakutana na timu ambayo ina wachezaji wazuri.

“Tumejipanga kiushindani kwa ajili ya mchezo huu, hivyo umakini unahitajika na tusipokuwa makini tunaweza kufungwa kizembe, lakini hata hivyo nimewaandaa vema wachezaji wangu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles