31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, NAMUNGO MALENGO SAWA

NA MWANDISHI WETU

TIMU Za Simba na Namungo leo zinatarajia kushuka dimbani kuumana, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho maarufuku Kombe la Azam, utakaochezwa Uwanja wa Nelson Mandela,Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mchezo huo utakuwa wa tatu kuzikutanisha timu hizo, baada ya kukutana mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, ambapo Simba ilishinda mchezo mmoja na mwingine zikitoka suluhu.

Timu hizo zitaingia uwanjani kila mmoja ikiwa malengo sawa na mwenzake, zikisaka rekodi na heshima.

Timu hizo kila moja inayo tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, Simba itaiwakilisha Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Namungo ikinasa tiketi ya Shirikisho Afrika.

Simba ilipata fursa hiyo baada ya kushinda taji la Ligi Kuu Bara msimu uliopita,huku Namungo ikikata tiketi baada ya kufika fainali ya Kombe la Azam ambayo itapigwa leo.

Kulingana na taratibu za Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), bingwa wa Ligi Kuu hupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati yule wa Kombe la Azam hushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini kama timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ndio iyo iyo iliyobeba ubingwa wa Kombe la Azam, basi timu iliyomaliza nafasi ya pili Kombe la Azam ndiyo itakayopata fursa ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hivyo basi, Namungo imejihakikishia kushiriki Kombe la Shirikisho kwakua hata kama itapoteza mchezo wa fainali dhidi ya Simba itaikwaa tiketi hiyo kupitia nafasi ya pili.

Kwakuzingatia mazingira hayo,Simba itaingia uwanjani ikihitaji ushindi ili kuweka rekodi ya kutwaa taji la pili kwa msimu huu .

Namungo wao kwa upande wao, licha ya kuwa ina tiketi mkononi ya Shirikisho Afrika, pia inaitaka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Azam, tena ukiwa msimu wake wa kwanza ikiwa Ligi Kuu.

Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 ilioupata,katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliochezwa Januari 29, mwaka huu Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam (zamani Uwanja wa Taifa).

Safari ya Simba kuelekea fainali ya michuano hiyo ilianza kwa kuichapa Arusha FC mabao 6-0, mchezo wa hatua ya 64 bora uliochezwa Disemba 21, mwaka jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ikaiondosha Mwadui kwa ushindi wa mabao 2-1, mchezo wa hatua ya 32 bora uliochezwa Januari 25, mwaka huu,Uwanja wa Mkapa.

Ilifuzu hatua ya 16 bora na kukutana na Stand United na kushinda penalti 3-2, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ua bao 1-1.

Ushindi dhidi ya Stand uliipeleka Simba robo fainali(nane bora)ambapo ilikutana na Azam na kushinda mabao 2-0, mchezo uliochezwa Julai Mosi.

Simba ilitinga nusu fainali za kukutana na Yanga na kuibukana ushindi mnono wa mabao 4-1, mchezo uliochezwa Julai 12, Uwanja wa Mkapa.

Namungo kwa upande wao, ilianza kuilaza Green Warriors bao 1-0,mchezo wa mzunguko wa 64 uliochezwa Disemba 22 mwaka jana Uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Ikaitungua Biashara United mabao 2-1, mchezo wa hatua ya 32 uliochezwa Januari 26 kwenye uwanja huo huo.

Ikatakata kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, mchezo wa hatua 16 bora uliochezwa Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Namungo ilitinga robo fainali baada ya kuifumua Alliance mabao 2-0, mchezo wa robo fainali uliochezwa Juni 30 mwaka huu, Uwanja wa Majaliwa.

Ushindi dhidi ya Alliance uliipeleka nusu fainali ambako ilikutana na Sahare All Stars na kuibuka na ushindi wa bao 1-0,

Mchezo uliochezwa Julai 11 Uwanja wa Mkwakwani,Tanga.

Kuelekea mchezo huo,Kocha wa Namungo , Hitimana Thiery amethibitisha kukosekana kwa mshambuliaji wake tegemeo, Relants Lusajo na beki Minza Kristom, kutokana na majeraha.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, lakini tumejiandaa kupambana kuhakikisha tunapata ushindi licha ya kuwa nitamkosa Lusajo na Minza,”alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Kwa upande wake,Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema amekiandaa vema kikosi chake kwa lengo la kushinda mchezo huo na kuweka taji la pili katika kabati lao msimu huu.

“Ni mchezo ambao tunahitaji kushinda hivyo tutatumia wachezaji wetu wote bora ili kuhakikisha tunashinda. Wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo.” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles