26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA NA YANGA ZILIVYOTAWALA USAJILI BONGO

Na MOHAMED MHARIZO-DAR ES SALAAM

UNAPOZUNGUMZIA soka la Tanzania huwezi kukwepa kuzitaja klabu za Simba na Yanga kutokana na ukongwe wao na pia kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kuliko klabu nyingine.

Pia Simba na Yanga ndizo klabu zenye mashabiki wengi zaidi kuliko nyingine, hata zinapokutana klabu hizi mashabiki hufurika uwanjani kushuhudia mahasimu hao wakichuana.

Hata msimu wa usajili wa Ligi Kuu Tanzania kwa klabu hizi hutikisa kutokana na kushindana katika kufanya usajili, ndio maana mashabiki wengi hufuatilia usajili wa Simba na Yanga zaidi kuliko klabu nyingine.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilifungua dirisha la usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kwa msimu wa 2017/2018 kuanzia Juni 15 mwaka huu na limefungwa Agosti 6, mwaka huu.

Tangu kuanza kwa usajili Simba na Yanga zilikuwa zikiviziana kusaka wachezaji watakaowatumia katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Simba ambao ni mabingwa wa Kombe la FA Tanzania (Azam Confederation Cup 2017), wataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, imefanya usajili wa wachezaji nyota kama John Bocco, aliyekuwa akiichezea Azam FC.

Bocco alisaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba baada ya kumalizana na Azam FC aliyoichezea kwa misimu 10 mfululizo.

Bocco amekuwa mshambuliaji tegemeo wa Azam FC akiiongoza kutwaa mataji likiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2014 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame mwaka 2015.

Pia Simba imeonekana kuibomoa Azam FC kwa kumsajili beki Shomari Kapombe kwa mkataba wa miaka miwili.

Ukiachana na Bocco na Kapombe, Simba haikuishia hapo, ilimnasa pia kipa namba moja wa Azam FC, Aishi Manula, huku pia ikimnyakua kiungo raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Usajili wa Niyonzima umeonekana kuitikisa Yanga, hakuna asiyefahamu uwezo wake, kila shabiki wa Tanzania anapenda kuona timu yake ikiwa na kiungo kama Niyonzima.

Pia Simba katika kujiimarisha zaidi imemrudisha kundini mshambuliaji wake wa zamani, Mganda Emanuel Okwi, ambaye ana uzoefu katika mashindano ya kimataifa.

Hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa Okwi kurejea Simba ambapo awali aliondoka na kujiunga na Etoile du Sahel ya Tunisia, baadaye aliachana na timu hiyo na kujiunga na Yanga ambapo alidumu kwa muda kabla ya kurudi Simba alipodumu kwa msimu mmoja na kutimkia Denmark na sasa anarejea tena Msimbazi.

Pia Simba imewasajili Jamal Mwambeleko, Hassan Mlipili, Mohamed Said, Erasto Nyoni, Ally Shomari, Salim Mbonde, Emmanuel Mseja na Nichlaus Gyan.

Kwa usajili huu uliofanywa na Simba chini ya kocha Joseph Omog, mashabiki wa timu hiyo wanaamini kutakuwa na ushindani wa kukabiliana na changamoto za ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara na pia Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga pia hawakuwa nyuma katika kufanya usajili, ikumbukwe kuwa mabingwa hao wa Tanzania Bara wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika.

Usajili ulioshtua zaidi mashabiki wa Simba ni kuona mshambuliaji wao mahiri, Ibrahim Ajib, akijiunga na watani wao Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.

Usajili wake umewashtua mashabiki wa Simba, kama ilivyokuwa kwa Niyonzima kujiunga na Simba, si jambo geni kuona timu hizi zikichukuliana wachezaji. Ni jambo ambalo limekuwa ni mazoea kufanyika katika usajili.

Lakini ukiachana na wachezaji hao, Yanga pia imesajili wachezaji wengine kama Rafael Daud, Papy Tshishimbi, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Rostand Youthe, Pius Buswita, Ramadhan Kabwili na Baruani Akilimali.

Yanga inayonolewa na kocha George Lwandamina, ina kazi ya kuonyesha uhodari wake kwa kuhakikisha inaendeleza rekodi yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia kufanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika.

Hivyo ni wakati wa Simba na Yanga kuonesha kuwa wao ni wakongwe katika soka la Tanzania kwa kufanya vizuri si katika Ligi Kuu Tanzania Bara, bali pia katika mashindano ya kimataifa ambayo watashiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles