NA MOHMED KASSARA -DAR ES SALAAM
KIKOSI cha Simba, leo kitashuka dimbani kuikabili Mtibwa Sugar, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi utakaochezwa kwenye Uwanja wa Aaman, Unguja.
Simba ilitinga hatua hiyo, baada ya kuwavua ubingwa Azam kwa ushindi wa penalti 3-2, timu hizo zilifikia hatua hiyo baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Ijumaa iliyopita kwenye uwanja huo.
Simba ilizindua kampeni zake za kulisaka taji hilo kwa kuichapa Zimamoto mabao 3-1, katika mchezo wa mtoano uliochezwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Mtibwa wao walianza harakati zao kwa kuitimua mashindanoni timu ya Chipukizi kwa kuilaza penalti 4-2, baada ya dakika 90 kumalizika kwa kufungana bao 1-1.
Wakata Miwa hao wa Morogoro, walitinga fainali baada ya kuitoa Yanga kwa penalti 4-2, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Simba imetinga fainali, ikiwa imepachika mabao matu na kuruhusu wavu wao kuguswa mara moja, katika michezo yake miwili, huku Mtibwa ikifunga mabao mawili na kuruhusu wavu wao kutikiswa mara mbili.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika michuano hiyo ilikuwa mwaka 2015, ambapo Simba ilitwaa taji hilo baada ya kuichapa Mtibwa Sugar kwa penalti 4-3 katika mchezo wa fainali.
Mtibwa itaingia uwanjani ikihitaji kushinda ili kulipa kisasi cha kupoteza fainali hiyo, lakini pia kumaliza hasira za kufungwa na Wekundu hao wa Msimbazi, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Septemba 13, mwaka jana, ambapo walilazwa mabao 2-1.
Mchezo baina ya timu hizo mara nyingi hutawaliwa na ufundi na mbinu, huku eneo la katikati ya uwanja na uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja vikipewa nafasi ya kubwa ya kuamua mbabe wa mtanange huo.
Simba na Mtibwa ni timu zinasifika kwa kutumia viungo wengi kwenye mchezo mmoja, hali ambayo ikiibuka vita kali hasa kati kati ya uwanja na yule anayekuwa bora zaidi eneo hilo anakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck amekuwa akitumia mfumo wa 4:2:3:1, ambao unajumuisha viungo watano na mshambuliaji mmoja, hivyo kukipa mamlaka kikosi chake ya kumiliki mpira zaidi na kumtawala mpinzani.
Hata hivyo, kazi haitakuwa rahisi kwake kwani kikosi cha Mtibwa chini ya Kocha Zuberi Katwila ambaye anapendelea kutumia mfumo wa 4:4:2 unaobadilika kwenda 4:3:3 wanapokwenda kushambulia.
Kutokana na uhodari wa viungo wa pande zote mbili, mpira unatarajiwa kuchezwa zaidi katikati ya uwanja, huku vita kubwa ikiwa kati ya Jonas Mkude, Sharaf Eldin Shiboub, Clatous Chama, Francis Kahata na Ibrahim Ajib dhidi ya Abdulhalim Humoud, Haruna Chanongo, Awadh Salum, Salum Kihimbwa na Awadhi Issa.
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanapata ushindi katika mpambano huo na kutwa taji hilo, ili kuongeza hamasa zaidi kwenye kikosi chao msimu huu.
“Mtibwa ni timu nzuri, inacheza mpira wa kasi na mashambulizi ya kushtukiza. Tunategemea kupata upinzani mkubwa katika mchezo wa fainali hapo kesho lakini lazima wajue Simba ni timu kubwa na tumejiandaa kuhakikisha tunatwaa taji hili la Mapinduzi.
Wachezaji wote tulio nao huku Zanzibar wapo tayari kwa ajili ya mchezo kwa hiyo ni sisi benchi la ufundi kuamua nani aanze na nani asubiri,”alisema Matola.
Kwa upande wake, Katwila alisema kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya kuikabili Simba na katika mchezo huo na kutwaa taji hilo.
“Tunajua tunakutana na timu nzuri, lakini tayari nimeaanda mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunakuwa makini zaidi na kupunguza makosa yanayoweza kutugharimu ili kuishinda Simba, tutahakikisha hatuwapi nafasi ya kutuadhibu,”alisema Katwila.