30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Simba kibaruani kuivaa Jamhuri

kikosi cha simbaNA MSHAMU NGOJWIKE, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba leo wanatarajia kushuka dimbani kutupa karata yao ya kwanza kwa kuvaana na timu ya Jamhuri ya Pemba katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Amaan.

Simba ambao wamepangwa Kundi A la michuano hiyo wataingia uwanjani saa 2:15 usiku kuwakabili wapinzani wao ikiwa ni baada ya mchezo wa awali wa JKU dhidi ya URA ya Uganda kupigwa kwenye uwanja huo jioni.

Kocha Mkuu wa Simba Mwingereza, Dylan Kerr ambaye atakinoa kikosi hicho kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Mapinduzi, amesema matokeo ya ushindi yatatokana na jitihada za wachezaji wake uwanjani kwani tayari amewapa majukumu.

Alisema anaamini michuano ya mwaka huu itakuwa migumu kutokana na ubora wa timu zinazoshiriki lakini wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza historia ya kulitwaa kombe hilo.

“Mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zinazoshiri, kwa upande wetu tumejipanga kwa matokeo mazuri ili kuendeleza historia ya kufanya vizuri kwenye michuano hii,” alisema.

Simba inajitupa uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao 1-0 iliopata dhidi ya Ndanda FC Ijumaa iliyopita katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa na historia nzuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa mara tatu wakifuatiwa na Azam FC waliochukua mara mbili huku Yanga, Miembeni, Mtibwa Sugar na KCCA wakilinyakua mara moja.

Simba walifanikiwa kutwaa taji hili mwaka jana baada ya kuifunga Mtibwa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Beki tegemeo wa Simba, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, ataikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi kutokana na kupata majeraha yatakayomfanya akae nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili.

Kutokana na kukosekana beki huyo, Kerr atalazimika kumtumia Emery Nimubona upande wa kulia ambaye alionyesha kandanda safi wakati timu hiyo ilipocheza na Ndanda wiki iliyopita.

Kiungo Jonas Mkude aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria uliomsababisha kukosa mchezo uliopita dhidi ya Ndanda, aliondoka na kikosi cha Simba kilichosafiri kwenda Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles