24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Simba isiwaogope, isiwapuuze wapinzani CAF

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF), Ijumaa iliyopita lilichezesha droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huko jijini Cairo nchini Misri.

Katika droo hiyo, wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo, timu ya Simba ilipangwa kundi D pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vital ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na J.S Saoura ya Algeria.

Mbali ya kundi la Simba, pia kuna makundi mengine matatu ambayo kila moja lina timu nne zinazofanya jumla ya timu zinazoshiriki hatua ya makundi ya michuano hiyo kuwa 16.

Kila kundi litatoa timu mbili ambazo zitafuzu hatua ya robo fainali itakayohusisha timu nane.

Ukweli ni kwamba, ukiondoa timu ya Saoura ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2008, Al Ahly na AS Vital ni timu zenye uzoefu wa kutosha katika michuano ya kimataifa ikiwemo Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ina maana kwamba, ili kupata nafasi moja kati ya mbili na kufuzu hatua inayofuata, Simba inatakiwa kupambana kweli dhidi ya wapinzani wake hao.

MTANZANIA tunafahamu kwamba Simba ina rekodi nzuri miongoni mwa timu za Tanzania inapocheza dhidi ya timu kutoka mataifa ya Kiarabu.

Na katika kundi lake, Simba itakutana na Al Ahly na Saoura ambazo ni timu kutoka mataifa ya Kiarabu.

Kutokana na rekodi yake, ni wazi wadau wengi wa soka na hasa wapenzi wa Simba watakuwa wamepata matumaini kuwa kikosi chake kitafanya vizuri na kutinga robo fainali.

Hata hivyo, pamoja na rekodi kudhihirisha makali ya Simba dhidi ya timu kutoka mataifa ya Kiarabu, bado hili halitoshi kuamua mustakabali wake katika hatua ya makundi ya michuano hii mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika.

Badala yake, kinachotakiwa kufanywa kwa sasa ni kwa uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na wapenzi wa Simba kuunganisha nguvu na kuweka mikakati makini itakayoiwezesha timu  yao kuvuka mtihani huo.

Na miongoni mambo ya msingi ya kufanyia kazi ni pamoja na kuhakikisha Simba inapata matokeo ya ushindi katika michezo yake yote itakayocheza nyumbani.

Tunalisema hilo kwa kuzingatia ukweli kwamba, timu nyingi za Kiafrika zimekuwa zikielekeza nguvu zake kuhakikisha zinapata ushindi katika ardhi ya nyumbani, huku ugenini zikifikiria zaidi katika kutafuta sare.

Kwa kuweka mikakati kabambe ikiwemo kuvuna pointi zote tatu nyumbani, tunaamini Simba ikataka tiketi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.

Pamoja na yote hayo, Simba haitakiwi  kuwaogopa wapinzani wake kwani kwa kufanya hivyo ni kama kukubali udhaifu.

Mara zote mshindi katika mchezo wa aina yoyote ukiwamo wa soka unategemea na ukubwa wa maandalizi yaliyofanywa na mchezaji au wachezaji.

Bahati nzuri, Simba ina kocha Patrick Aussems ambaye tayari ameonyesha uwezo wake mkubwa wa kukifanya kikosi cha timu hiyo kuandika rekodi mpya katika michuano ya kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles