NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
WEKUNDU wa Msimbazi Simba kama wataamua kuleta mzaha katika usajili wa dirisha dogo, basi isahau suala la kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, bado haijawa kwenye fomu yake kama ilivyokua misimu mitatu iliyopita, licha ya kujitutumua kutaka kurudi kwenye nafasi mbili za juu ambazo ilikua ikipishana na mahasimu wao Yanga.
Timu hiyo ina nafasi mbili pekee za kuweza kuongeza wachezaji kwenye usajili huu wa dirisha dogo, hivyo wanahitaji kuwa makini katika kupata wachezaji hao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Said Tully, alisema hawataki kufanya usajili ambao utawagharimu na kuweza kukwamisha harakati zao za kumaliza katika nafasi nzuri kwenye ligi kuu msimu huu.
“Tumekuwa kimya tukitafakari wachezaji tutakaowaongeza katika nafasi hizo, tunataka kujiridhisha hasa na aina ya wachezaji tutakaowasajili kabla ya kuwapa mikataba.
“Tutafanya usajili wetu kwa kushirikiana na kocha ili kuongeza wachezaji ambao ataridhika na kiwango chao, hatutasajili bila yeye kuridhika kwani tunaweza kusajili mshambuliaji kumbe yeye hitaji lake ni kwa beki hivyo tutakuwa hatumsaidii,” alisema.
Simba kabla ya ligi kuanza ilikua na hitaji la mshambuliaji, matokeo yake wakaleta washambuliaji ambao hawakidhi haja ya timu.
Awali walimleta Msenegal, Papa Niang, ambaye hakufanya vizuri akatupiwa virago vyake na kuondoka, ndipo akasajiliwa Msenegal, Pape N’daw ambaye hadi sasa ameonekana garasa na anatajwa kutemwa katika usajili wa dirisha dogo na Mganda Simon Sserunkuma.
Wakati uongozi unajipanga hayo tayari mchezaji Paul Kiongera amepewa asilimia kubwa za kutua kwenye kikosi hicho ikiwa ni kuziba nafasi ya Simon Sserunkuma ambaye tayari ameshatemwa rasmi kuchezea kikosi hicho huku Pape N’daw naye akiwa njiani kutemwa.