23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simba hakuna kulala

Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

BAADA ya kuchukua pointi tatu, jijini Mbeya, kikosi cha Simba kinatarajia kuanza mazoezi leo  kujiandaa na mechi ijayo dhidi  ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Jumamosi hii, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Simba imetua jana Dar es Salaam ikitokea Mbeya ilikocheza na Ihefu mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kushinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ushindi huo umewafanya Wekundu wa Msimbazi hao, kuendeleza ubabe Ligi Kuu Bara kama sehemu ya harakati zao za kutetea ubingwa wao.

Baada ya kuwasili jana, wachezaji walipewa mapumziko na leo jioni wanatarajia kuanza mazoezi katika uwanja wao wa Mo Simba Arena, uliopo Bunju, jijini. 

Akizungumzia mchezo wao na Ihefu, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema ulikuwa mgumu lakini kitu muhimu kwao ni pointi tatu walizozipata.

Alisema siku moja kabla ya mechi hiyo, aliwaambia wachezaji wake, bila kujali watakutana na changamoto gani, muhimu ni kupambana kupata alama tatu na wamefanikiwa.

“Nilikuwa natarajia mchezo mgumu, Ihefu ni mechi yake ya kwanza Ligi Kuu na inakutana na Simba, hivyo niliwaambia wachezaji wangu haijalishi ni jinsi gani tutashinda, lakini pointi tatu ni muhimu.

“Nafurahi tumeanza na pointi tatu, ni mwanzo mzuri kucheza ugenini na kurudi nyumbani na pointi tatu, ligi ni ngumu tutazidi kujipanga,” alisema Sven.

Sven alisema kwa sasa anachanga karata zake jinsi ya kuikabili Mtibwa Sugar kwa sababu anafahamu ni kati ya timu ngumu, hivyo watafanya maandalizi mazuri.

Naye Kocha Mkuu wa Ihefu, Maka Mwalwisi, alikiri kuwa wamecheza na timu kubwa inayopigania kutetea ubingwa wake na kwamba haikuwa mechi rahisi.

“Tumecheza na timu kubwa ambayo ni mabingwa, ina wachezaji wazoefu, unapofanya kosa moja, wanakuadhibu na ndicho kilichotokea,” alisema Mwalwisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles