Theresia Gasper -Dar es salaam
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, leo wanatarajia kushuka dimbani kuumana vikali na Power Dynamic ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa tamasha la ‘Simba Day’.
Tamasha hilo ambalo ni la 10 tangu kuanzishwa kwake, limekuwa likifanyika kila Agosti 8, lakini msimu huu imekuwa tofauti kutokana na klabu hiyo kubanwa na ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba wataitumia mechi hiyo ya leo kama maandalizi ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, unaotarajiwa kuchezwa Agosti 10, mwaka huu ugenini.
Mechi ya marudiano itapigwa Agosti 25, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lakini pia, Wekundu wa Msimbazi hao wataitumia nafasi hiyo leo kutambulisha wachezaji wao wapya waliowasajiliwa hivi karibuni.
Wachezaji wapya walionaswa na Simba ni Tairone Santos, Gerson Fraga na Wilker Henrique da Silva (Brazil), Francis Kahata (Kenya), Sharaf Eldin Shiboub (Sudan) na Deo Kanda (DR Congo), huku wazawa wakiwa ni Kennedy Juma (Singida United), Gadiel Michael, Ibrahim Ajib na Beno Kakolanya (Yanga) na Miraji Athuman (Lipuli FC).
Wageni hao wameungana na wenyeji, wakiongozwa na nahodha John Bocco, wengine wakiwa ni Aishi Manula, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Clatous Chama, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Yusuph Mlipili, Rashid Juma, Ally Salim na Hassan Dilunga.
Mashabiki wa Simba watakuwa na shauku ya kushuhudia viwango vya wachezaji wao wapya kutokana na usajili uliofanywa, ukizingatia timu hiyo imepania kuweka rekodi katika michuano ya kimataifa.
Timu hiyo iliweka kambi Afrika Kusini ya wiki mbili na kucheza mechi nne za kirafiki, dhidi ya Orbert Tvet na kupata ushindi wa mabao 3-0 kabla ya kuichapa Platinum Stars mabao 4-1.
Katika mchezo mwingine, walitoka sare ya bao 1-1 na Township Rollers na kumalizia na sare nyingine kama hiyo dhidi ya Orlando Pirates.
Akizungumzia mchezo huo wa leo na dhidi ya UD Songo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema wamefanya maandalizi ya kutosha hivyo wanaamini watafanya vizuri.
“Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi wakiwa wamevaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe kuisapoti timu yao na kuwaona wachezaji wapya waliosajiliwa,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescetius Mgori, alisema tukio lao la leo litaweka historia.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, amewaongoza wachezaji wa timu hiyo kutoa msaada katika kituo cha Makao Makuu ya Watoto Yatima Kurasini, Dar es Salaam.
Mfanyabiashara huyo ametoa msaada wa sh milioni 10 ambazo zitatumika kununua mashine za kutotolea mayai, huku pia akiahidi kuwagharamia majengo ya kushi watoto 100, msaada huo ukiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Simba Day.
Akizungumza na viongozi, watoto wanaoishi kwenye kituo hicho na wachezaji wa Simba, Dewji alisema anatambua kuwa watoto hao wanapitia katika kipindi kigumu, hivyo msaada huo utasaidia kuboresha maisha ya watoto wanaoishi kwenye kituo hicho.
Alisema msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli za kuboresha maisha ya Watanzania na yeye kama mfanyabiashara ambaye anaunga mkono juhudi za serikali, anaamini ana wajibu wa kusaidia kusaidia jamii inayomzunguka na hasa watu wenye uhitaji, wakiwapo yatima.
“Mimi najua hata Mhe. Rais atapenda jambo hili kwamba mimi nagharamia mwenyewe na hela zao zote za matumizi nitatoa mimi. Na pia, najua wanahitaji kupata sehemu ya malazi, mtakaa mkubaliane, sisi tutakuja kujenga majengo kwa ajili ya hao watoto 100 wakae.
“Tunataka tuzidishe watoto yatima, kwahiyo tutatafuta hao watoto 100, Taasisi ya Mo Dewji itawagharamia. Lakini la pili, tutajenga miundombinu ili watoto waishi kwenye mazingira mazuri na la tatu nitatoa sh milioni 10 ili zitumike kufanya biashara ili watoto waishi kwenye mazingira mazuri na bora zaidi,” alisema Dewji.
Baada ya kutoa ahadi hiyo, Dewji aliwataka wachezaji wa Simba kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya watoto hao kwa kila mchezaji kuwa na watoto watatu ambao atawasimamia na kwa kila mchezaji kutakiwa kukutana na watoto ambao anawasimamia angalau mara moja kwa kila miezi mitatu.
Akitoa taarifa kuhusu kituo hicho, Ofisa Mfawidhi wa Makao Makuu ya Watoto Kurasini, Beatrice Laurence, alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha mipango yao ya kuwa na biashara ambazo zitawawezesha kujiendesha.
“Tunashukuru sana kwa msaada ambao umetupatia, ambao utasaidia kuboresha maisha ya watoto ambao tunaishi nao hapa kituoni. Ni wazi sasa kwamba maisha ya watoto hawa yatabadilika,” alisema.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1975 na kwa sasa kinatunza watoto 72 ambao wengi wao ni wadogo na wengine wanasoma shule za msingi, sekondari na baadhi chuo kikuu.