26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, COASTAL NI VITA YA WABABE

Theresia Gasper -Dar es salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa michezo saba kupigwa kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Simba wataikaribisha Coastal Union Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba itaivaa Coastal ikitoka kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wapinzani wao Coastal watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya bao 1-1 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mkwakwani jijini Tanga dhidi ya Biashara United.

Timu hizo zilipokutana msimu uliopita, Simba ilishinda

mabao 2-1 mzunguko wa kwanza, mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani,  Tanga kabla ya Wekundu hao kupata ushindi mnono wa mabao 8-1, mzunguko wa pili kwenye dimba la Uhuru, Dar es Salaam.

Simba ndiyo vinara wa msimamo wa ligi hiyo wakijikusanyia pointi 44 katika mechi 17 walizocheza hadi sasa, wakishinda michezo 14, sare mbili na kupoteza mmoja.

Coastal wao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 30, baada ya kushuka dimbani mara 17, wakishinda mara tisa, sare tatu na kupoteza mechi tatu.

Simba itashuka dimbani ikihitaji kuendeleza ushindi ili kuzidi  kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Coastal mbali ya kutaka kuvuna pointi tatu ili kuzidi kujongea juu ya msimamo, itaingia uwanjani na fikra za kutaka matokeo mazuri ili kujitibu jeraha za kutandikwa mabao 8-1.

Michezo mingine ya ligi hiyo leo itakuwa kati ya Namungo ambayo itairibisha Mbao dimba la Majaliwa Lindi, Ndanda itapepetana na Alliance Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Kagera Sugar wao watakuwa nyumbani Uwanja wa Kaitaba Kagrea kuumana na Singida United, wakati ambao Biashara United itapimana ubavu na Mwadui dimba la Karume, Mara.

Ruvu Shooting itavutana mashati na Lipuli Uwanja wa Mabatini,  Pwanim, Tanzania Prisons  itakabiliana na KMC dimba la Jamhuri, Dodoma.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven VanderBroeck,  alisema kila mechi wanahitaji ushindi hivyo lazima wafanye vizuri na kuendelea kujiweka katika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi.

“Katika mechi zetu zilizopita niliona wachezaji wangu wakichoka mapema lakini nimewaweka sawa ili wasifanye makosa kama hayo tena,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Coastal, Juma Mgunda alisema wamejipanga vizuri kupata ushindi ili kujipoza machungu ya kupoteza mechi zote mbili msimu uliopita

“Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kwani Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri lakini hata sisi kikosi chetu kipo vizuri na tumejipanga kiushindani,” alisema Mgunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles