Simba, Bandari Mombasa kupimana ubavu

0
749

MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

KLABU ya Simba imethibitisha kuwa, Oktoba 12, mwaka huu kikosi chake kitacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya Bandari Mombasa ya nchini Kenya.
Benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems kinataka kuutumia mchezo huo kukiweka sawa kikosi chao kabla ya kurejea kwenye mikiki mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Oktoba 23 itashuka dimbani Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam  kuikabili Azam FC.

Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa muda kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Mchezo huo utakuwa wa tatu katika kipindi hiki cha kalenda ya Fifa, awali uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kuwa kikosi chao kitacheza michezo ya kirafiki dhidi ya timu ya Ligi Kuu Burundi ya  Aigle Noir na Mashujaa FC, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza .

Mchezo kati ya Wekundu hao na Aigle utapigwa Oktoba 14, wakati dhidi ya mashujaa  utarindima Oktoba 16, yote ikichezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu alithibitisha timu hiyo kucheza michezo hiyo kwa lengo la kukiweka sawa kikosi chao katika mbio za kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara.

Alisema huo utakuwa utaratibu endelevu  wa kucheza michezo ya kirafiki katika kipindi cha mapumziko ya ligi,  ili kuwapa fursa mashabiki wa timu hiyo kuiona timu yao mikoani.

“Ni kweli tutacheza michezo hiyo mitatu ya kirafiki na tutakuwa tukifanya hivi kila mapumziko yanapotokea, lakini tutakuwa tukicheza na mabingwa wa nchi tofauti ili kuwapa mashabiki wetu ladha kama kipindi tunashiriki michuano ya kimataifa.

“Baada ya kucheza na Bandari, ratiba inaonyesha tutaondoka Oktoba 13 kwenda Kigoma kucheza michezo miwili dhidi ya Mashujaa na Aigle Noir, kisha tutasubiri ripoti ya kocha kuona kama tunaweza kuicheza mchezo mwingine kabla ya kuivaa Azam,” alisema Rweyemamu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here