24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, AZAM RAHA TU

Waandishi Wetu

SIMBA imerejea kwenye mstari, baada ya kuilaza Mtibwa Sugar, mabao 3-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Ikumbukwe kuwa, kabla ya kuumana na ‘Walima miwa’ hao, Simba ilipoteza mchezo wake dhidi ya JKT  Tanzania, baada ya kuchapwa bao 1-0.

Wakati Simba ikichanua, vigogo wengine wa soka hapa nchini, timu ya Azam nayo ilitakata baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, katika mchezo ambao pia uliochezwa jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco dakika ya 45, Mohamed Hussein ‘Tshababala’, dakika ya 47 na Hassan Dilunga dakika ya 58.

Bocco alifunga bao lake kwa mguuu wa kushoto, baada ya kupokea pasi ya Meddie Kagere na kuwazidi maarifa mabeki wa  Mtibwa.

Tshabalala kwa upande wake alifunga lake, baada ya kuwazidi kasi mabeki wa Mtibwa na kutandika shuti lililomshinda kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado, wakati Dilunga alipachika bao baada ya kupokea pande la Bocco.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kujikita kileleni, ikifikisha pointi 53, baada ya kucheza mechi 21, ikishinda 17, sare mbili na kupoteza mbili.

Kipindi cha kwanza, licha ya kila upande kufanya mashambulizi, Simba ilionekana dhahiri kuzitaka pointi tatu.

Dakika ya pili Dilunga akianza kuitikisa ngome ya Mtibwa kwa shuti lilidakwa na Kado.

 Mtibwa alijibu kupitia Haruna Chanongo, aliyepiga shuti lakini likatoka nje la lango la Simba.

Dakika ya 16, kiungo Francis Kahata alichonga pasi safi kwa Bocco ambaye alishindwa kufunga baada ya kiki yake kuishia mikononi mwa Kado.

Dakika ya 21, Bobani Zirintusa, alishindwa kuipa Mtibwa uongozi, baada ya kupata pasi ndefu ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na kuachia mkwaju uliodakwa na kipa wa Simba, Aishi Manula.

Dakika ya 26, kiungo Jonas Mkude aliachia fataki iliyotoka pembeni mwa lango la Mtibwa kabla ya dakika ya 28,  mshambuliaji Stamili Mbonde kumtoka beki wa Simba,Tairone Santos na  kuachia kiki iliyopanguliwa na Manula.

Mashambulizi ya Simba, yalizaa matunda dakika ya 45, baada ya Bocco akiwa kwenye msitu wa mabeki wa Mtibwa kufunga bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika.

Kipindi cha pili Simba, ilichachamaa zaidi kwa kuzidisha kasi ya mashambulizi langoni mwa Mtibwa.

Presha ya Simba iliifanya Mtibwa kukosa utulivu kwani wachezaji walijikuta wakitumia muda mwingi kuzuia kuliko kushambulia.

Dakika ya 47, Tshabalala alifunga bao la pili kwa upande wa Simba.
Kuona hivyo, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Zuber Katwila, alifanya mabadiliko dakika ya 53, alimtoa, Juma Luizio na kumuingiza, Salum Kanoni.

Hata hivyo, Mtibwa ilijikuta ikifungwa bao la tatu lililowekwa wavuni na Dilunga dakika ya 58.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbloeck kumtoa Bocco dakika ya 74 na  kumwingiza, Luis Miquissone.

Pamoja na Mtibwa kujikakamua kutaka kurejesha mabao, dakika 90 zilikamilika kwa Simba kuvuna pointi tatu.

Kwa upande mwingine, kiungo Mudathir Yahya aliing’arisha Azam kwa kuifungia bao pekee lililoipa ushindi dhidi ya Polisi Tanzania.

Michezo mingine ya ligi hiyo iliyopigwa jana, Ndanda iliifunga Mwandui mabao 2-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mabao ya Ndanda yalifungwa na Samwel John dakika ya 69 na Omary Hamis dakika ya 89.

Singida United ikiwa nyumbani ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Namungo, mchezo uliopigwa Uwanja wa Liti.

Bao la Namungo lilifungwa na Zingamasebo  Steven dakika ya 68.

Dimba la Karume mjini Musoma, Biashara United ilishinfa bao 1-0 dhidi ya Mbao.

Bao la Biashara lilipachikwa na Atupele Green dakika ya  63.

Lipuli ililazimishwa na sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania, Uwanja wa Samora Iringa, Kagera Sugar ikachapwa mabao 2-1 na Alliance FC, Uwanja wa Kaitaba Bukoba.

Mabao ya Alliance yalifungwa na Martin Kigi dakika ya 64 na David Richard 90.

Bao pekee la Kagera likifungwa na Nassor Kapama.

Wakati huo huo mchezo kati ya Ruvu Shooting na Tanzania Prisons, ambao pia ulikuwa huchezwe jana  Uwanja wa Mabatini Pwani, ulihirishwa baada ya gari ya huduma ya kwanza kuchelewa kufika.

Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alithibitisha hilo kwakusema gari lililopaswa kutumia lilipata dharura ya kumkimbiza mgonjwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles