25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Simanzi yatawala mazishi aliyechomwa na mume wake

Andrew Msechu-DAR ES SALAAM

NI simanzi. Ndivyo unaweza kusema,baada ya mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kukusanyika na kushiriki mazishi ya Naomi Marijani, ambaye anadaiwa kuuawa na mume wake, Khamisi Luwongo, kisha kuteketeza mwili wake kwa kuuchoma moto.

Inadaiwa Naomi, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Mei, mwaka huu, ambapo picha na taarifa zilizodaiwa kuandaliwa na mumewe Luwongo, zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai atakayefanikisha kupatikana kwake, atapa zawadi ya Sh milioni moja.

Kutokana na taarifa hizo ambazo baadaye, Kamanda Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Amon Kakwale,  alisema Mei 19, mwaka huu, Luwongo alifika katika Kituo cha Polisi Gezaulole, Kigamboni na kufungua jalada la taarifa kuwa mkewe, Naomi ametoroka.

Alisema kama ilivyo taratibu za polisi, walianza uchunguzi  na Juni 12, Luwongo alifika tena kituoni hapo na  kueleza kuwa mke wake, ametelekeza mtoto wao anayeitwa Grecious (7).

Jana ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Naomi, walikusanyika nyumbani kwa kaka yake Mbweni, Dar es Salaam na kufanya ibada wa mazishi kama ishara ya kutimisha msiba wake.

Katika ibada hiyo, pia ilihudhuriwa na majirani wa Naomi waliokuwa wakiishi naye Kigamboni pamoja na vikundi mbalimbali vya kwaya.

Akizungumza wakati wa ibada hiyo ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa alilokuwa akisali marehemu Naomi la Sabato Gezaulole,  Jackob Chimbwegu, alisema wakati wote wa uhai wake marehemu alikuwa mshirika mzuri ambaye alisababisha kununuliwa kwa viti vya kisasa plastiki.

“Tumeguswa sote, kwa kilio cha maumivu mliyonayo ndugu, hakuna namna ya kuwatuliza. Zaidi ni kumwomba Mungu awatulize mnaopita katika wakati huu mgumu,” alisema Mchungaji Chibwengu

Pamoja na hali hiyo, aliwataka waombolezaji kujiweka tayari kuonana na Mungu kwa kuwa katika maisha ya binadamu ni mafunzo tosha, kwani hakuna anayejua atakavyoondoka hapa duniani.

Naye Mchungaji Emmanuel Mhando wa Kanisa la FPCT, alisema kuna maswali mengi watu wanaweza kujiuliza, kwa nini Naomi, kwa nini kifo kiwe cha namna hii?

Alisema kwanini zinakuwa nyingi, lakini hakuna haja ya kulalamika tena, hakuna haja ya kujiuliza, bali kuomba nguvu ya kusonga mbele.

“Ni imani yangu baada ya ibada hii, tusiendelee kulaumu, tuseme inatosha, inatosha, tumuombe Mungu atupe nguvu ya kusonga mbele,” alisema Mchungaji Mhando

KAULI YA FAMILIA

Kwa upande wake,msemaji wa familia, Wiseman Marijani alisema jambo lililowasibu ni zito na gumu wakati wote walikuwa wamezongwa na hawakujua nini cha kufanya.

Alisema familia inapenda kumshukuru Mungu kwa mambo makuu,  tangu Naomi aliyedaiwa kupotea Mei 15, mwaka huu, lakini wakaja kujua aliko siku 60 baadaye.

“Tulianza kukata tama, Mungu alitufungulia fumbo na kujua aliko Naomi, baada ya mbingu kumlazimisha Meshack, mumewe kueleza kinagaubaga kuhusu ukatili alioufanya, alisema.

Alisema anaushukuru uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi, vyombo vya habari pamoja na wananchi ambao walisaidia kupata taarifa za haki aliko Naomi.

Alisema taarifa zilizosaidia kujulikana aliko Naomi zilipatina kutoka kwa msamaria ambaye aliwapa mbinu iliyosaidia kutanzua fumbo hilo

Alisema kwa kuwa suala hilo liko mahakamani, wanaiombea mahakama iweze kutoa haki stahiki.

Alisema baada ya ibada maalumu kufanyika jana, familia itaendelea kusubiri mamlaka husika ili ziwarejeshee mabaki ya mwili wa Naomi ili waweze kumpumzisha kwa amani.

TAARIFA ZA KUUAWA

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Amon Kakwale alisema baada ya utata wa taarifa za tukio hilo, polisi walianza utaratibu wa uchunguzi  ambapo Juni 12, Luwongo alifika tena kituo hicho cha polisi na kueleza kuwa Naomi ametelekeza mtoto anayeitwa Grecious mwenye umri wa miaka saba.

Kamanda huyo alisema baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa hizo, kesi hizo zilianza kufanyiwa kazi.

Alisema wakati wanaendelea na uchunguzi juu ya suala hilo, ndugu wa Naomi nao walifika katika kituo cha Polisi Chang’ombe, wakieleza kuwa ndugu yao alikuwa amepotea na wana shaka na mumewe kuhusu kutoweka kwake.

Alisema kutokana na maelezo hayo ya ndugu wa Naomi, Jeshi la Polisi likamtia mbaroni Luwongo kwa ajili ya mahojiano.

Alisema Julai 15, akiwa mbele ya jeshi hilo akaeleza taarifa alizokuwa ameeleza awali hazikuwa za kweli na akaanza kueleza ukweli wa namna mkasa mzima ulivyokuwa.

Julao 30, mwaka huu, mume aliyekuwa akishikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe, kisha kumchoma kwa mkaa magunia mawili ya mkaa na kumzika shambani kwake, Khamisi Luwongo (Meshack), alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Luwongo, alifikishwa mahakamani hapo na kuwekwa mahabusu ya mahakama hiyo akisubiri kupangiwa Hakimu.

Hata hivyo, jalada la kesi  ya mauaji ya kukusudia limepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Mmbando.

Mshtakiwa  anatuhumiwa kumuua mkewe Naomi (36), Mei mwaka huu katika maeneo ya Kigamboni,Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles