SIKU YA MAZINGIRA: SERIKALI INAVYOCHOCHEA HARAKATI UHIFADHI VYANZO VYA MAJI

0
997
Vijana wakiosha mchanga katika Mto Ruvu ili kupata madini ya Dhahabu

 

 

Na Mwandishi Wetu,

JUNI 5 ya kila mwaka Watanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. 

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliamuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu mazingira huko Stockholm, nchini Sweden. 

Aidha, Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme, UNEP, lilipitishwa pia siku hiyo.

Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka Juni 5, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.

Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yahusuyo mazingira, pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali duniani kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira.

Aidha, Serikali hutumia siku hii kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika mazingira na kuyafanya yawe salama na masafi ili kufurahia hali hiyo katika maisha na vizazi vijavyo.

Mwaka huu, kimataifa maadhimisho haya yanafanyika nchini Canada. Uamuzi wa kupeleka maadhimisho haya nchini Canada ni kutokana na nchi hiyo  kuwa na maeneo mengi yenye mazingira asili  ya ardhi na maji ukilinganishwa na nchi zingine.

Kitaifa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yalifanyika mkoani Mara, Butiama.

Kauli mbiu inaliyoongoza maadhimisho hayo kimataifa ni ‘Connecting People to Nature.’ Kwa Kiswahili ni: ‘Uhusiano Endelevu Kati ya Binadamu na Mazingira.’ Kaulimbiu hii inahamasisha jamii kuwa na urafiki endelevu na mazingira asilia ambapo kila mtu anapaswa kutambua, kufurahi, kujivunia na kulinda uzuri wa mazingira asilia na kuhamasishana kuyatunza na kuyahifadhi.

Pamoja na kaulimbiu ya kimataifa, kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira mwaka huu kitaifa ni ‘Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda.’ Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira wakati wa kukuza maendeleo ya viwanda nchini.

Hata hivyo, miaka ishirini baadae mkutano mwingine wa kilele ulifanyika huko Rio de Jeneiro nchini Brazil, ambao pia uliweka changamoto kubwa katika suala la ulinzi, usimamizi na utumiaji endelevu wa mazingira na rasilimali zilizopo. Hivyo, baada ya mkutano wa  Rio, jukumu la kuhifadhi, kulinda na kusimamia kikamilifu utunzaji wa mazingira na matumizi ya rasilimali duniani limepewa kipaumbele na Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshighulikia Mazingira (UNEP).

Aidha, maudhui ya Siku ya Mazingira katika sekta ya maji ambapo inakadiriwa kwamba ikiwa kasi ya matumizi ya rasilimali na uzalishaji itaendelea kama ilivyo, wakati idadi ya watu inakadiriwa kufikia bilioni 9.6 mwaka 2050, zitahitaji sayari Dunia (the mother earth) tatu ili kukidhi mahitaji ya binadamu (UNEP, 2012). Hivyo, kaulimbiu ya Siku ya Mazingira nchini  inahimiza wananchi kutambua umuhimu wa kutunza rasilimali  za maji kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mahitaji ya maji katika sekta ya kilimo yanaongezeka kwa kasi kubwa kutokana na ongezeko la  uwekezaji wa viwanda maeneo ya mijini, watu na maendeleo ya kiuchumi. Kwa sasa matumizi ya maji safi duniani kote ni zaidi ya mara mbili tangu Vita Kuu ya II ya Dunia na inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia nyingine 25 ifikapo mwaka 2030. Kilimo kinachukua zaidi ya theluthi mbili za matumizi ya maji ya kimataifa, ikiwa ni takribani asilimia 90 katika nchi zinazoendelea. Idadi ya watu duniani inatarajiwa kuongezeka kutoka bilioni 6.6 kwa sasa na kufikia bilioni 8 ifikapo mwaka 2030 na zaidi ya bilioni 9.6 ifikapo mwaka 2050.

Kupitia Wizara ya Maji, Serikali imekuwa ikihakikisha kunakuwapo na sera, miongozo, sheria na mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba rasilimali hii inatunzwa, pia inapatikana kwa ajili ya matumizi ya wananchi wake.

Sera na Sheria za Maji, lengo kuu la sera ya maji ni kuendeleza sekta ya maji kwa ajili ya maendeleo endelevu katika usimamizi wa rasilimali za maji kwa kuweka mifumo madhubuti ya kisheria na kitaasisi katika utekelezaji.

Aidha, sera inalenga kuhakikisha kwamba wadua wote wanashiriki kikamilifu katika mipango, ujenzi, uendeshaji, matengenezo, usimamizi na usambazaji wa miradi ya maji ndani ya jamii. Pia sera inaweka misingi endelevu ya usimamizi wa rasilimali za maji kwa kubadili majukumu ya Serikali kutoka katika jukumu la kutoa huduma za maji na kuendelea na jukumu la  uratibu, na uundaji wa sera, miongozo na kanuni kwa ajili ya utekelezaji.

Hivyo, sera hiyo inatekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (2006-2025). Aidha, utekelezaji wake unasimamiwa na Sheria Na. 11 ya mwaka 2009 ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji pamoja na Sheria Na. 12 ya Mwaka 2009 ya Utoaji wa Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira.

Moja ya eneo la mto Ruvu ambalo ni chanzo cha maji ya Ruvu Juu eneo la Ruvu Darajani.
Utekelezaji katika kutunza vyanzo vya maji, chanzo cha maji ni eneo linaloweza kuhifadhi maji yanayoweza kutumika kwa matumizi ya viumbe hai akiwamo binadamu kwa muda wote wa mzunguko wa maji wa msimu wa mwaka (hydrological cycle). Kwa hapa Tanzania tunayo mito maziwa, chemchemi, mabwawa (asili na kujengwa) visima, maeneo chepechepe, yanayoweza kuwa na sifa kama hizo.

Rasilimali ya maji duniani ni ile ile haiongezeki na kinachotokea ni maji kuwa katika hali zake tatu tofauti hali ya ugumu (barafu), maji (kimiminika), hewa (mvuke). Kwa kusaidiwa na nguvu za jua maji kutoka baharini huchukuliwa kwa njia ya mvuke hadi angani na kupoozwa kuwa mawingu, nayo mawingu huchukuliwa na upepo hadi maeneo ya uwanda wa juu ya bahari na maziwa kwenye milima yenye misitu.

Hivyo, yafikapo maeneo hayo huanza kunyesha mvua na ifikapo juu ya ardhi hukusanywa katika mabonde na mito na kurejea tena katika maziwa na mwisho baharini. Aidha, mengine huzama katika udongo na kujitokeza baadaye kama chemchem  ambazo pia huendeleza mito ya kudumu.

Sehemu ya maji hayo huenda chini katika miamba ya mbali kadiri ya mita 50- 100-600 na kufanya akiba ya maji ya ardhini. Maji haya huweza kupatikana tena kwa njia ya visima. Katika mzunguko huu ndipo tunapata vyanzo vya maji baridi  kadri mzunguko huo unavyoendelea.

Katika ramani ya maji, Tanzania imegawanywa katika mabonde tisa ambapo Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(DAWASA) huchukua maji yake katika Bonde la Wamiruvu.

Meneja wa Usimamizi Uendeshaji na Mazingira wa DAWASA, Modester Mushi anasema mamlaka hiyo ni miongoni mwa zile zilizo chini ya bonde hilo na imekuwa ikishirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ya bonde iliyopo mkoani Morogoro katika kutekeleza baadhi ya majukumu yake, haya yakiwa ni pamoja na yale ya kulinda vyanzo vya maji.

Msimamizi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na mambo mengine, ana jukumu la kusimamia utunzaji wa vyanzo, ulinzi wa mazingira, ushirikishwaji wa wananchi katika kutunza vyanzo na mazingira na ugawaji wa rasilimali zote za maji katika eneo la bonde.

Ushiriki wa DAWASA kupitia ofisi za bonde la Wami Ruvu huwa katika maeneo mbalimbali  kama vile kushirikiana na vikundi vya wananchi vilivyounda jumuiya za watumia maji katika kuwapa mafunzo, kupanda na kutunza miti yenye kuhifadhi uoto wa asili na ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Hadi sasa maelfu ya miti imepandwa kwa kushirikisha jamii ndani ya maeneo yenye vyanzo vya Mto Ruvu ambapo kwa jinsi miaka inavyosogea, muitikio wa wananchi na viongozi katika kuonyesha uhitaji wa kupanda miti unaendelea kuongezeka na hii ni dalili nzuri kuwa uelewa wa umuhimu wa kuhifadhi mazingira unaongezeka siku hadi siku.

Hivyo, DAWASA ni mshirika wa karibu katika harakati za utunzaji wa mazingira hasa vyanzo vya maji ili viweze kuendelea kuzalisha maji yanayotegemewa na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here