33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SIKU YA FIGO DUNIANI: UNENE ULIOKITHIRI UNACHANGIA KUHARIBIKA KWA FIGO

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa watu milioni 600 duniani wameathirika na unene uliokithiri (wengi wana viribatumbo au vitambi).

Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Idara ya Lishe Februari mwaka huu, katika maadhimisho ya wiki ya lishe unaonesha kuwa asilimia 39.9 kati ya watu waliojitokeza kuchunguza hali ya lishe walikutwa na uzito uliokithiri (obesity) wakati asilimia 29.5 walikuwa na uzito mkubwa (over weight).

Wataalamu wanaeleza kwamba unene uliokithiri ni miongoni mwa sababu kuu inayochangia watu wengi leo hii kuugua magonjwa ya figo.

Sababu

Daktari Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Watoto, anayesoma uzamivu katika magonjwa ya figo ya watoto na watu wazima katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Herrieth Sissya anasema kuna sababu nyingi zinazochangia hali hiyo kutokea.

“Unene uliokithiri husababisha matatizo ya figo ama moja kwa moja au unaweza kusababisha vitu vingine ambavyo baadae husababisha tatizo la figo. Mtu anapokuwa mnene seli za mafuta ambazo huwa tumboni, kitaalamu zinaitwa ‘visceral fat’ hutoa vichochezi ambavyo baadae huwa na athari hasi katika figo.

“Vichocheo hivi huathiri muundo na utendaji kazi wa vichujio vya figo. Kwa hiyo, unapokuwa na unene uliokithiri muda mrefu figo hulazimika kufanya kazi zaidi ya kawaida kutokana na uzito kuwa mkubwa kulinganisha na figo ambayo hubaki na ukubwa ule ule.

Kinachotokea

“Kawaida figo huwa haiongezeki, mtu akiongezeka mwili yenyewe hubaki na ukubwa ule ule, kwa hiyo figo hulazimika kufanya kazi ya ziada ya kutoa taka mwili hivyo huenda ikifa taratibu,” anasema.

Anatoa mfano; “Tuchukulie watu wawili, mmoja ana kilo 20 mwingine ana kilo 100 wakavaa viatu kwa muda sawa sawa, yule mwenye uzito wa kilo 20 cha kwake kitadumu wakati wa kilo 100 kitawahi kuisha.

Dk. Sissya anataja sababu nyingine kuwa ni magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu hasa la juu na magonjwa ya moyo.

“Magonjwa haya kwa namna moja au nyingine hutokana na unene uliokithiri ingawa pia yanarithiwa, mtu anaweza kuzaliwa nayo.

“Kwa hiyo magonjwa haya matatu mgonjwa akiyapata na kukaa nayo muda mrefu na asipate matibabau baadae nayo humsababishia magonjwa sugu ya figo katika maisha yake,” anasema.

Dawa za kienyeji, kichina na maumivu

Daktari huyo anasema matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu nazo huchangia mtu kupata magonjwa ya figo.

“Mtu akijisikia maumivu anakimbilia dukani si jambo sahihi lazima uzitumie kwa ushauri wa daktari, lakini pia wengine wanakunywa dawa za kienyeji na kichina (za kuongeza maumbile) ambazo kimsingi huwa hazitolewi kwa kuzingatia vipimo.

“Mtu anapewa tu akatumie matokeo yake wanaishia kuziumiza figo zao bila wenyewe kujua,” anasema.

Aina za magonjwa ya figo

Dk. Muhiddin Abdi Mahmoud anasema yamegawanyika katika aina mbili ambayo ni magonjwa ya figo ya dharura na sugu, yote ni hatari kwani husababisha figo kushindwa kufanya kazi.

Anasema magonjwa ya dharura ni hatari zaidi kwani mwili huwa na mkusanyiko mkubwa wa sumu wa papo kwa hapo.

“Magonjwa ya maambukizi ni sababu kuu inayosababisha magonjwa ya figo ya dharura, kwa mfano malaria; mtu akiugua na asipate matibabu ya haraka hugeuka kuwa malaria sugu hatimaye kuathiri figo.

“Kitendo cha mtu kupoteza damu nyingi, mfano wanaopata ajali au wajawazito hali hiyo husababisha msukumo wa damu kuwa mdogo mwilini na figo inapokosa mzunguko wa kutosha huumia,” anasema.

Hali ni mbaya

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa MNH, Jaqueline Shoo anasema takwimu zinaonesha tatizo linaendelea kuwa kubwa duniani.

Anasema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10 ya watu duniani tayari wanaugua ugonjwa sugu wa figo na kwamba inakadiriwa ifikapo 2025 asilimia 70 ya wagonjwa watakuwa wanatokea katika nchi zilizopo katika ukanda wa Jangwa la Sahara.

Wanaotibiwa Muhimbili

Anasema katika kliniki yao wanaona wagonjwa wengi kila mwezi wakiwamo watoto.

“Tunapokea watoto kati ya 30 hadi 40 kila mwezi ambao wanaugua magonjwa ya mshtuko na asilimia 60 ni sugu.

Anasema wanaona watu wazima 120 hadi 150 kila mwezi.

Anasema; “wagonjwa 220 wamepandikizwa figo tangu mwaka 2006 hadi 2017 na wote wapo hai wanaendelea vizuri, wagonjwa 132 wanafanyiwa ‘dialysis na asilimia 50 kati ya hawa wapo kwenye mchakato wa kupandikiza figo, wanatafuta watu watakaowasaidia kupata figo ya kupandikizwa.

 “Mwaka 2011 WHO ilieleza kwamba Watanzania 4,300 kila mwaka hugundulika kuwa wanaugua magonjwa ya figo.

“Na kati yao wengi wanafariki kwa sababu ya magonjwa ya moyo, ndiyo maana tunaona kuna umuhimu wa kuelimisha jamii kupambana kupunguza visababishi vinavyochangia mtu kupata magonjwa haya hasa unene uliokithiri,” anasema.

Simulizi ya Asia na Meriat

“Hakuna kitu kingine unachohitaji kuwa nacho zaidi ya moyo wa upendo na huruma ili uweze kutoa kiungo chako kimoja kumpa mwingine iwapo inawezekana kufanya hivyo na wewe kubakiwa na kimoja.”

Haya ni maneno ya Meriat Siraji, ambaye anaishi na figo moja kwa miaka 10 sasa tangu alipoamua kujitolea kumsaidia ndugu yake Asia Mustapha ili aishi.

Ilikuwaje

Asia ni binti aliyekuwa na ndoto za kufika mbali kimasomo, alizaliwa akiwa hana tatizo lolote la kiafya hata hivyo akiwa kidato cha tatu mwaka 2005 mambo yalibadilika.

Asia anasema alianza kusumbuliwa na kikohozi cha mara kwa mara ambapo wazazi wake walilazimika kumfikisha hospitalini kupata matibabu baadae hali hiyo ilitulia.

Anasema hata hivyo baada ya muda mchache hali hiyo ilianza kujitokeza tena, akashauriwa na daktari mmoja wa Hospitali ya Hindu Mandal afanyiwe vipimo kuchunguza iwapo anasumbuliwa na magonjwa ya moyo.

“Kuna siku nilizidiwa hadi kupoteza fahamu, sikujua kwanini hali ile ilinitokea lakini nilifikishwa hospitalini na nilipochunguzwa iligundulika figo zangu (zote mbili) zimeharibika,” anasimulia.

Anasema haikuwa rahisi kupokea matokeo hayo lakini ilimlazimu na alimshukuru Mungu kwani ana makusudi yake.

“Madaktari walinishauri nianze huduma ya kusafishwa figo (dialysis), nilifanyiwa upasuaji mdogo nikawekewa mpira kwa ajili ya kuanza kupata huduma hiyo, ilipofika Mei, mwaka huo niligundulika nina tatizo la moyo,” anasema.

Anasema alipatiwa matibabu dhidi ya ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua na kwamba alipona kabisa.

Anasema baada ya kupona tatizo hilo alipatwa tena na tatizo la usikivu (ukiziwi). Aliendelea kupata huduma ya dialysis katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) huku akiendelea kutafuta ndugu wa kumsaidia kupata angalau figo moja.

“Katika kipindi chote hicho ndugu walijitokeza lakini tulipofanyiwa vipimo majibu yalionesha tulikuwa hatuendani.

“Sikukata tamaa niliendelea na matibabu ya dialysis hadi mwaka 2008 ambapo Meriat alijitokeza na vipimo viliendana hivyo akawa tayari kunisaidia kupata figo moja,” anasema.

Safari ya India

Anasema walisafiri pamoja hadi India ambako alifanyiwa upasuaji na kupandikizwa figo, furaha ya maisha ikarejea.

Meriat anasema; “nilipopata taarifa za ugonjwa unaomsumbua Asia nilijisikia huzuni hivyo niliamua kumsaidia.

“Naweza kusema ni ujasiri na msukumo nilioupata kutoka ndani ya moyo wangu, niliposikia habari juu ya ndugu yangu kuwa anahitaji figo angalau moja ili aweze kuishi vema.

“Sikujiuliza mara mbili, sikuona ulazima wa kumwambia mtu mwingine maana niliamini wangekuwapo wa kunikatisha tamaa, niliona kwanini ndugu yangu afe ikiwa ninao uwezo wa kumsaidia, nikafanya uamuzi,” anasema.

Wengi hukwepa suala hilo

Hili lipo wazi, wagonjwa wa figo wanaohitaji kupata mchangiaji hujikuta wakibakia wenyewe na kutengwa na jamii zao.

Hofu ya kutokuzaa

Meriat anasema sababu kuu inayowafanya watu wengi kuogopa kuwapa figo moja ndugu zao na kuwaacha wakiteseka ni kupoteza uzazi.

“Wanahofu kwamba wakitoa figo moja kizazi kitaharibiwa, jamii bado inahitaji kuelimishwa juu ya suala hili, hakuna ukweli wowote kwamba kizazi kinaharibika, mimi nimempa ndugu yangu figo moja, nimebakiwa na moja, sina tatizo lolote.

 “Muhimu ni kwamba nazingatia masharti niliyopewa na madaktari hasa kunywa maji ya kutosha na kupima afya mara kwa mara, namshukuru Mungu kwani amenijalia kupata mtoto mmoja, sasa naitwa mama,” anasema.

Changamoto

Asia anasema mwaka 2009 figo aliyopandikizwa ilianza kusumbua tena akapewa dawa ambazo zilimsaidia na maisha yakaendelea.

“2010 niliweza kujiunga na masomo ya QT, ili niweze kutimiza ndoto yangu ya kupata elimu lakini sikufanikiwa kumaliza kutokana na mazingira,” anasema.

Asia anasema baadae aliweza kujifunza kozi maalumu ya uhasibu kwa njia ya kompyuta ambayo inanisaidia kuendesha maisha yangu hivi sasa.

“Ilipofika mwaka 2011 figo niliyopandikizwa iliharibika kabisa. Hivi sasa nimerudi tena kwenye huduma ya kuchuja damu, bado sijakata tamaa, namshukuru Mungu kwani figo ile ilinisaidia kuishi miaka mitano na naamini nitapata ndugu mwingine atakayenisaidia kupata figo nyingine,” anasema kwa ujasiri.

Ni janga

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Muhimbili, Jaquiline Shoo anasema magonjwa ya figo nchini ni janga la kitaifa kwani idadi ya wagonjwa ni kubwa.

“Ni janga kwa sababu linaathiri uchumi wa nchi, yanadhoofisha wananchi ambao wanategemewa nguvu zao zitumike kujenga nchi, matibabu ya figo yanatumia gharama nyingi, serikali inalazimika kutumia fedha nyingi za pato la Taifa kutibu wananchi wake,” anasema.

Anasema kwa kuwa bado huduma za upandikizaji figo zinafanyika nje ya nchi serikali hufadhili matibabu hayo.

“Lakini sasa ina mpango wa kuanzisha huduma hii nchini ili kuokoa gharama na kuwezesha wananchi wengi kutibiwa,” anasema.

Kuhusu maadhimisho

Anasema Alhamis ya pili ya kila mwezi Machi dunia huadhimisha Siku ya Figo, lengo kuu likiwa ni kuihamaisha jamii ijikinge dhidi ya magonjwa hayo.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ambayo tumepewa na Chama cha Madaktari wa Figo Duniani inasema; ‘Mtindo bora wa Maisha, Afya bora ya Figo’. Katika harakati za kuyapunguza tunataka kupambana na vyanzo,” anasema.

Anaongeza; “Watu waishi katika mtindo bora wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles