33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Siku nane usajili laini za simu mwiba kwa Nida

NA FLORENCE SANAWA -MTWARA

ZIKIWA zimebaki siku 8 kabla ya mwisho ya kusajili laini za simu kwa alama za vidole, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameigeuzia kibao Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kwa maelezo kuwa wanakwamisha wananchi kupata namba za vitambulisho ili waweze kusajili laini zao.

Awali Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), ilitangaza kuwa mwisho wa kusajili laini kwa alama za vidole ni Desemba 31, mwaka jana.

Hata hivyo Desemba 27, Rais Dk. John Magufuli alitangaza kuongeza siku 20 kuanzia Januari mosi ili wananchi wengi waweze kusajili laini zao.

Kwa mujibu wa TCRA, hadi Desemba 13 mwaka jana, laini zilizokuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole ni 19,681,086 sawa na asilimia 42.

Ilisema pia laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole ni 21,782,906 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 10.5.

Wakati hayo yakiendelea, Lugola ameonekana kuwageuzia kibao Nida kwa kuchelewesha watu kupata namba za vitambulisho vya taifa ili waweze kujiandikisha.

Juzi akiwa Mtwara, Lugola alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk. Arnold Kihaule, kufika mkoani Lindi ili atoe maelezo kwanini asiwajibishwe kutokana na kusuasua kwa uandikishaji vitambulisho vya uraia, huku akitoa onyo kwa Ofisa Usajili Nida Mkoa wa Mtwara, Gide Magila na kumtaka kusambaza vitambulisho vyote walivyo navyo ofisini kwao.

Kauli hiyo ameitoa juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Mtwara.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu watendaji wa Nida kutoa lugha zisizofaa kwa wananchi wanaofika kutaka huduma hiyo. 

 “Wananchi wanatoa machozi kuwa watumishi wa Nida wana lugha kali, ni wasumbufu, haiwezekani machozi ya wananchi waliomchagua Rais John Magufuli yakawalilia watu wa Nida ilihali nao ni watumishi kama wengine, natuma salama kwa wafanyakazi wote wa Nida ambao hawataki kuchunga ndimi zao.

 “Haiwezekani Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ambayo imeshindwa kutoa vitambulisho vya uraia, wamekaa wanafanya mzaha na kucheza na kusababisha wananchi wanashindwa kusajili laini zao kwa alama za vidole.

“Wanafanya mzaha, hatutaruhusu zoezi hili ambalo Rais amejua umuhimu wa mawasiliano kwakuwa tunapata kodi kwenye miamala na vocha za simu, alafu wananchi washindwe kusajili laini kwa kukosa namba zao, muda huo hatuna tena, ndiyo maana nimemtimua ofisa Nida Ruvuma nimekuta ana namba za wananchi hajawapa.

 “Hata mkoa huu wa Mtwara nimekuta namba za utambulisho 2,954 watu hawajapewa tangu Desemba mwaka jana na ofisa amesema atagawa namba hizo leo leo na usipozigawa hizo namba kesho ndio itakuwa mwisho wa kazi yako ukalime matikiti.

 “Kwakweli watendaji Nida watakaoshindwa kuchunga ndimi zao wawajibishwe, hatuwezi kusimamia wananchi ili wapate vitambulisho vya uraia huku wengine wakitoa lugha zisizofaa na kufifisha zoezi hilo, mfano leo nimefika Nida nimekuta wananchi wengi, lakini watendaji hawapo ofisini, tusiruhusu wachache wanaochezea kazi kukwamisha zoezi hili,” alisema Lugola.

Akiwa Ruvuma, Lugola alimvua madaraka ofisa wa Nida wa mkoa huo, Seif Mgonja kwa kutogawa kwa wananchi Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN), 14,493 tangu Desemba 31 mwaka jana licha ya kuzalishwa na makao makuu na kupelekwa ofisini kwake mjini Songea.

Pia alimwondoa madarakani Ofisa wa NIDA Wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Thobias Nangalaba kwa kutofika katika kikao chake cha viongozi wa mkoa na wilaya, licha ya kupewa taarifa ya kuhudhuria kikao hicho. 

 “Ndugu wananchi wa Songea, maofisa hawa wamekuwa wakienda kinyume na maagizo ya Serikali ya kuwataka waweze kuwakamilishia wananchi usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kwa wakati, hivyo hawatufai na wanapaswa watupishe ili wengine waweze kuiongoza Nida mkoani hapa.

“Haiwezekani ofisa wa Nida mkoa anacheza na wananchi kwa kutopeleka taarifa ili waweze kupata fursa ya kusajili laini zao  ambapo zoezi hilo linatarajia kukamilika Januari 20, mwaka huu,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles