31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

SIKU KALAMU YA MWANAHABARI ITAKAPOVUNJIKA!

NA JAVIUS KAIJAGE                |                       


Kwa miaka ya karibuni pamekuwapo na hali inayotia shaka kwa namna uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari inavyozidi kusongwa kote duniani katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ripoti ya mwaka 2018 ya waandishi wa habari  wasio na mipaka (RSF) ilionesha wasiwasi huo kiasi kwamba hata mataifa ambayo hapo awali yalikuwa yakichukuliwa kuwa ni vinara wa uhuru wa kujieleza hususani nchi za Ulaya lakini na huko uhuru umeendelea kushuka.

Nchi nne  za Ulaya ambazo hali ya uhuru wa vyombo vya habari imeshuka ni Jamhuri ya Czech, Malta, Slovakia na Serbia.

Wakati huko Ulaya Uhuru wa vyombo vya habari ukiendelea kutiwa doa na hivyo kuharibu taswira na utamaduni ambao ulikuwa  umezoelekea kuwa wenzetu huko  ni waungwana kwa kuheshimu Uhuru na mawazo ya watu, hata Taifa kubwa la Marekani ambalo hujiita kuwa ni kiranja wa kutetea haki za binadamu bado kuna kuzaliwa mazingira ya kitisho dhidi ya vyombo vya habari.

Tangu aingie madarakani Rais Donald Trump ameonekana kutokuwa na urafiki dhidi ya vyombo vya habari kwani amekuwa ni kiongozi ambaye muda mwingi ni kuvilaumu vyombo vya habari kuwa havimtendei haki.

Haki anayohitaji Rais Donald Trump kutoka kwa vyombo vya habari inashangaza kwani kazi ya vyombo si kumfagilia kiongozi au kumkandamiza bali kuhabarisha jamii kwa kila kitu kinachotokea na kuendelea katika eneo husika kwa kuzingatia matakwa ya taaluma hiyo.

Si tu kuhabarisha jamii bali pia vyombo vya habari vinao wajibu wa kufundisha, kukosoa, kutafsiri na kuburudisha kulingana na muktadha wa tukio.

Kama mataifa ambayo kimsingi yalikuwa yanategemewa kuwa dira, ramani na kioo katika kuulinda uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari hali inaonekana kuchechemea,  Je, huku kwetu Afrika ambako kuna tawala nyingi zinazoendesha watu wake  kwa kutumia mkono wa chuma mambo yatakuwaje?

Taifa lipi litasimama na kukemea uchafu wa kuwapiga waandishi wa habari na kuwaharibia vifaa vyao kama ilivyotokea hivi juzi  nchini Uganda wakati wanataalumna hao  wakiripoti tukio la  wananchi kuandamana wakishinikiza  mbunge wao kuachiwa huru?

Nani atasimama na kukemea tawala mbovu huko Eritrea, Djibouti na Ethiopia ambako kwa mujibu wa ripoti ya waandishi wasio na mipaka ya mwaka huu imeonesha kuwa uhuru wa vyombo vya habari uko kitanzini?

Je, ni taifa lipi litasimama na kukemea tawala mbovu ambazo kwa kutaka kuficha uovu wao hasa katika kupora rasilimali za wanyonge mara nyingi zimekuwa  hazihitaji kumulikwa na vyombo vya habari?

Je, ni shirika lipi, taasisi ipi itasimama kidete kuwalinda na kuwatetea waandishi wa habari wanapokuwa wanaripoti katika mazingira ambayo kuna migogoro ya kisiasa hadi kusababisha mapigano  mfano  nchi za Afrika?

Je, waandishi wa habari  watakuwa tayari kupinga tawala mbovu ambazo kimsingi hazihitaji kung’atuka huku zikiendelea kukandamiza demokrasia bila ya uwepo wa mataifa yenye nguvu katika ujenzi imara wa vyombo vya habari?

Je, kama hali itaendelea kuwa mbovu duniani kote kuna haja  waandishi wa habari kubadili  uelekeo na mifumo ya ufundishaji katika ngazi zote kugeuzwa  na kuanza kufundisha kuwa kazi ya uandishi wa habari ni kutii mamlaka bila kuhoji chochote?

Je, waandishi wa habari  wakiamua kususia kila kitu na kubaki  kimya bila kuandika chochote  katika magazeti au kutangaza kwenye luninga na redio dunia itakuwaje?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles