30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

SIDO KUSIMAMIA UANZISHWAJI VIWANDA KILA WILAYA

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KATIKA kuhakikisha azma ya Tanzania ya viwanda inatimia, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), linahamasisha viongozi wa wilaya zote nchini kuchangamkia Mkakati wa wilaya moja bidhaa moja (ODOP) ili kuongeza uzalishaji na upatikanaji ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Profesa Sylvester Mpanduji, alisema lengo la kuanzishwa shirika hilo ni kuendeleza viwanda vidogo nchini hivyo mkakati wa ODOP ni moja ya jukumu lao kubwa na watalisimamia ili waone likifanikiwa.

“Lengo la mkakati huu tuliouanzisha mwaka 2007, ni kuhamasisha wilaya kutumia rasilimali walizonazo ili kuanzisha viwanda, tunafahamu Tanzania ina ardhi nzuri kwa kilimo na kila wilaya ina zao linalostawi vema.

“Hivyo wananchi wakishirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya kulima, kuvuna na kuongezea thamani zao husika na kuliingiza sokoni naamini kutakua na tija kubwa baada ya miaka michache na nchi nzima itakua na viwanda vidogo vinavyozalisha bidhaa zenye ubora unaofaa kimataifa,” alisema Profesa Mpanduji.

Akitolea mfano Mkoa wa Morogoro wenye wilaya saba, Profesa Mpanduji alisema: “Wilaya ya Morogoro Vijijini wamechagua zao la tangawizi, wilaya za Morogoro Mjini na Mvomero wamechagua kuchakata mafuta ya alizeti, Kilombero na Ulanga wamechagua mchele, wakati wilaya za Kilosa na Gairo wamechagua asali na nta ya nyuki,” alisema.

Alibainisha kuwa mkoa huo unafanya kazi vizuri na wananchi wanachangamkia fursa zilizopo katika kila bidhaa wanazochakata wakati Sido kazi yao ni kutoa elimu juu ya masoko na teknolojia ya kuongezea thamani mazao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo na Huduma za Mikoa Sido, Joyce Meru, aligusia suala la wananchi kuchangamkia fursa lakini pia kushauri viongozi wa wilaya kuchagua mazao wanayoona yanastahili katika maeneo yao ili kuongeza ajira.

“Mpango huu ulianza rasmi mwaka 2010, baada ya kukaa miaka mitatu tangu mwaka 2007 tukitoa elimu juu ya namna ya kutumia mashine na kutambua fursa. Tulibaini kila wilaya ikiwa na kiwanda itakua rahisi kuwaepusha vijana kukimbilia mjini ambako fursa za ajira zinazidi kupungua.

“Kwa mfano Wilaya ya Same wananchi walichagua zao la tangawizi, tuliwasaidia kuweka mashine za uchakataji katika kiwanda chao na sasa nadhani ni miongoni mwa wilaya zinazofanya vizuri katika usindikaji zao hilo,” alisema Meru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles