23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

SIASA ZA DAMU NI HATARI KWA MUSTAKABALI WA NCHI YETU


Na DK. GEORGE KAHANGWA  |  

KWA mara nyingine tena, Taifa letu limefikwa na wingu la simanzi, majonzi na hofu kutokana na vifo vya Watanzania wenzetu vilivyotokea katika mazingira yanayohusiana na siasa.

Makala hii ni sehemu ya tafakuri ya kilichojiri na maombolezi ya vifo hivyo. Makala inajaribu kutoa neno la faraja, kukemea vitendo vyote vilivyolisababishia Taifa matukio ya umwagaji damu na mauaji.

Aidha, makala inalionya Taifa juu ya hatari inayotukabili endapo hatutaweka ukomo wa siasa mbovu nchini.

Pengine si la kusisitiza sana (maana linajulikana) kwamba Tanzania ni Taifa la watu wanaomjua na kumheshimu Mungu.

Ni Taifa ambalo kila uchao kupitia wimbo wa Taifa, linamwomba Mungu aibariki nchi, abariki viongozi wetu na atubariki wana wa kike na wa kiume.

Wanasiasa walioko katika Taifa linalosali sala ya namna hiyo, hawana budi kutambua kwamba wao pamoja na raia wengine, wana wajibu wa kutiii amri za Mungu ambazo ni pamoja na kutokuua.

Hakika Taifa linalomjua Mungu haliwezi kushindwa kutambua kuwa damu isiyo na hatia inapomwagika juu ya ardhi hugeuka kuwa laana juu ya nchi husika.

Misahafu imeliweka wazi hili inaposema:‘Basi sasa umelaaniwa wewe katika ardhi iliyofumbua kichwa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako’. Utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake.

Biblia katika kitabu cha Mwanzo 4:11-12 Na pengine imeandikwa; ‘Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, ni kwa ajili ya Sauli na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni (2 Samwel 21:1)’.

Kama Taifa, tunapaswa kuhakikisha laana hii ya kujitengenezea haiachwi ikashamiri na kutamalaki, eti kwa sababu tunafanya siasa.

Hatuna budi kuwaambia waziwazi wanasiasa na mashabiki wao walioshiriki kumwaga damu yatosha sasa, watubu kwa Mwenyezi Mungu awasamehe na waombe radhi kwa Watanzania wote.

Wakati Watanzania tunaendelea kuziombea roho za Marehemu waliouawa Zanzibar mwaka 2001 na za Marehemu Godfrey Luena (aliyekuwa diwani wa Namwawala), Akwilina Akwilini (aliyekuwa mwanafunzi wa DIT), Alphonse mawazo, Daudi Mwangosi na wengine waliouawa katika muktadha wa kisiasa, ingefaa tuwaone wanasiasa wakikutana pamoja kufanya toba na wakija mbele za Watanzania kujutia kwa dhati haya waliyoyasababisha.

Pasi na kufanya hivyo, wanasiasa wote wenye mkono katika hili, hawastahili kutuongoza, hawastahili kufika kwa wananchi kuwaomba kura; hawastahili kupanda katika jukwaa lolote la kisiasa huku damu za ndugu zetu zikiwalilia.

Vile vile wanasiasa hawa hawana uhalali wa kuzungumzia maendeleo wakati mikono yao imejaa damu na imeijaza mioyo ya wafiwa majonzi yasiyomithilika.

Bila toba ya dhati, wanasiasa wa namna hii watambue sasa, kwamba wameshakataliwa si tu na wananchi, bali na Mungu mwenyewe kama alivyowakataa wanasiasa waliokuwapo katika vizazi vilivyopita wakawatendea watu maovu.

Hao wa zamani walifanya machukizo hadi Mungu akawatumia ujumbe wa MENE MENE TEKELI NA PERESI (Biblia: Daniel 5: 24–31).

Ni dhahiri wanasiasa wanaomwaga damu, Mungu ataweka ukomo kwenye uongozi wao; amezipima siasa zao na kubaini zina upungufu mkubwa.

Hivyo, mamlaka aliyowapa wanasiasa hawa (hata kama bado wanakalia viti vya kisiasa), amekwishayagawa kwa watu wengine walio wema.

Ndiyo, yamegawiwa kwa watu wengine wanaojua thamani ya uhai wa mtu na wako tayari kuulinda kwa gharama yoyote ile. Tunao watu katika Taifa hili ambao wako tayari kukosa madaraka ya kisiasa ili uhai wa mtu ulindwe.

Bali wale wanasiasa ambao wako tayari Watanzania waangamie ili wao wachache waendelee kupata utukufu wa kisiasa, hawafai maana hakika asili yao ni kwa baba wa uovu.

Tanzania ni nchi inayostahili baraka, lakini badala yake baadhi ya wanasiasa kazi yao ni kututengenezea laana. Tanzania inastahili siasa za kutunza amani, utengamano na uhai wa kila kiumbe, lakini wanasiasa waovu wameona watuingize kwenye siasa za damu na mauti!

Tuwaangalie wanasiasa hawa, kwamba Nabii wa Mungu alipata kuonya hivi; “Angalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu, shina la uchungu lisije likachipua na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo (Waebrania 12:15)’  Baadhi ya wanasiasa wetu, kwa siasa zao za damu na mauti, wamejipunguzia neema ya Mungu.

Wamesababisha kuchipua kwa shina la uchungu katika nchi iliyosifika kwa miaka mingi katika amani na utulivu. Wanakotupeleka sasa wanasiasa hawa ni katika shina hili kuisumbua nchi na wanatuongoza Watanzania wote katika kupata unajisi.

Kwa hiyo, kabla hawajatufikisha huko, sisi Watanzania tunapaswa kuwakemea kwa nguvu zote, washindwe katika nia yao ovu ya kuinajisi nchi.

Watanzania hatuko tayari kuwa kama Somalia, Kongo au Syria ambako wanasiasa kama hawa wa kwetu (baadhi) waliendekeza ulevi wa vikombe vya madaraka yaliyojaa damu na sasa mataifa haya yanaogelea katika mabwawa ya damu pasi na matumaini yoyote ya kurejea katika amani.

Huko Syria walianza kidogo kidogo mwaka 2011 kwa kuilalamikia Serikali, miaka sita baadaye bado wana vita vya ndani visivyoelekea kukoma. Somalia walianza kumwaga damu hivi hivi miaka ya 1980, sasa ni miaka takribani 38 bado Taifa lao halieleweki.

Shime Watanzania, tukemee aina hii ya siasa zilizoibuka nchini. Aidha, nawashauri Watanzania wote popote walipo, kuchukua tahadhari za usalama maana yanayofanywa na wanasiasa ni mchezo wa furaha kwao lakini mauti kwetu.

Tuendelee kuwaambia waziwazi (wanasiasa hawa) wote waliohusika na siasa za kuua ndugu zetu kwamba hatuna imani nao. Ingefaa waache unafiki wa kufika misibani, kutuma salamu za pole na fedha za rambirambi zinazonuka damu.

Kwa wanasiasa mnaoendelea na siasa safi (au wanaodhani hawajashiriki dhambi hii), wana wajibu wa kuthibitisha usafi wao kwa kuifanya ajenda ya kulinda uhai wa Mtanzania kuwa hoja yao ya kipaumbele cha kwanza, popote watakaposimama kuhutubia au popote watakapokaa katika vikao vya uamuzi. Tanzania isiyo na siasa za kumwaga damu, isiyo na wanasiasa wanaosababisha vifo vya raia (ili wao wafanikiwe) inawezekana.

Mwandishi ni Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Anapatikana kwa namba; +225 713 563 212

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Uandishi wa kioga, Uandishi usio na maana, Usio na ukweli, uandishi kama story tu bila undani. Kama unataka kuadika hadithi fanya hivyo. Lakini kama wewe ni mwandishi wa mafunzo andika ukweli wa wa mambo. Nani alimmpiga Mwongosi si siasa ni mtu. Nani alimipga Aquilina ni mtu na wanajulikana na si siasa.
    Nani alimteka ulimboka walijulikana ni taasisi na jina lao si siasa. Nani alifyatua risasi hadharani, si siasa ni mtu wa taasisi. Mnatumia siasa bila kuandika ukweli wa mambo ili kutoa picha isiyo sahihi kwa wananchi. Mko wengi wenye majukumu mnashindwa kusimamia karamu zenu ingawa mwandishi mwenzenu bado kapotea. Woga wenu ndo unaozipa nguvu hizi taasisi na Watu wachache kudhurumu na kuwafumba watu midomo. Mbona mwanamuziki Diamond anawatetezi wengi. yeye ni mwana muziki tu, Lakini nchi hii inashindwa kuungana kutetea mambo ya muhimu zaidi kwa Watanzania wote kama Katiba, uonezi wa kisiasa, Elimu kwa mabinti wapewao mimba na Wanaume, Elimu bora, na kunyanyaswa kwa Waandishi, Kutekwa ovyo, kusimamia haki za maiti za Wananchi zinazookotwa Kusimamia mali zetu na mikataba mibovu, Ufisadi. . Watanzania Wasomi wazima wameshindwa kuungana kwa pamoja kukumea na kupiga stop mambo haya. Haya ni mabaadhi ya mambo makuu yanayolikabili Taifa letu kwa mara ya kwanza, Uhuru wa kutoa mawazo, kukutana. Watanzania wamekuwa kondoo vichwa chini kama hawana elimu na uwezo wa kufikiri. Kuna wenye MAPHDS, Masters of Dedrees, Wote chali.
    Faida za usomi ni ni nini. Kukusanywa kama kondoo au mmambuzi. Ni aibu kwa Taifa letu kuwa kondoo wasio na uwezo wa kufikiri wakimsujudia mtu mmoja kama Mungu.Mungu kazi yake kutamka tu.viwe na vinakuwa. How,

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles