Si sahihi mzazi kuingilia uamuzi wa mtoto anayejielewa

0
1136

Na CHRISTIAN BWAYA

FIKIRIA wewe ni kijana mwenye ndoto fulani binafsi, unashauku ya kufanya kitu fulani maishani, lakini wazazi wako hawakuungi mkono kwa sababu kuna kitu wanachokitaka wao bila kujali utashi wako. Ungejisikiaje? Fikiria umefikia umri wa kutafuta mwenzi wa maisha. Kuna mtu unafikiri angefaa kuwa mume/mke wako lakini wazazi wako hawako tayari kuona unafunga ndoa na mtu huyo.

Chukulia tayari unafamilia yako lakini huwezi kufanya uamuzi unaohusu familia yako bila kutafuta idhini ya wazazi wako kwa sababu hawawezi kufurahia kuona unafanya chochote bila kuwashirikisha. Ungejisikiaje?

Kama wewe ni huna tofauti na wengine, uwezekano ni mkubwa hutajisikia vizuri hata kama hutakuwa na namna nyingine. Ni kwa sababu kuna mambo kama binadamu tungependa kuyafanya bila kuingiliwa na watu wengine, wakiwemo wazazi wetu. Hii haimaanishi kuwawajuaji au kutokutaka ushauri bali ni ile hali ya kujisikia unauhuru Fulani wa kufanya mambo kwa kujitegemea.

Kwanini basi inakuwa vigumu kwa wazazi kuwaacha watoto wafanye uamuzi wao wenyewe bila kuwaingilia? Kwanini hawapendi kuwapa watoto nafasi ya kuamua mathalani, wakasome nini bila kuwamulia? Kwanini mtoto hawezi kuamua afanye nini maishani bila kumwelekeza nini cha kufanya? Kwanini baadhi ya wazazi wako tayari hata kuingilia maisha ya watoto wao ambao tayari wanafamilia zao?

Sababu zipo nyingi lakini iliyokuwa kubwa ni kule kutokuamini kuwa watoto wanaweza kuamua jambo sahihi bila wao kufahamu. Kuna yale mazoea ya wazazi kufikiri pasipo watoto kuwategemea maana yake hawafanyi wajibu wao. Ingawa ni vizuri kuwa na tahadhari na kuwasaidia watoto kuamua kadri inavyohitajika. Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kwamba wajibu wa mzazi ni kumjenga mtoto kuwa mtu anayejitegemea anayeweza kufanya uamuzi mwenyewe tena sahihi, bila ya kutegemea ushiriki wa watu wengine.  Mzazi anayetaka mtoto awe tegemezi kwake, mtoto asifanye kitu kisicholingana na matarajio yake, mtoto asiamue mambo yanayoendana na utashi wake binafsi, mzazi huyu anaweza kujikuta akilazimika kuingilia uamuzi wa watoto hata watakapokuwa watu wazima.

Naelewa katika umri fulani, huwezi kumwachia mtoto afanye vile apendavyo. Mtoto anahitaji kusaidiwa kukua chini ya uangalizi wa mzazi, ambaye kwa kawaida huwa na uelewa na uzoefu zaidi kuliko mtoto. Lakini hata hivyo, ni muhimu kuzingatia pia kuwa kujenga mazoea ya utegemezi uliopindukia ni tatizo.

Tabia ya kupenda kuwadhibiti watoto mara nyingi hutokana na ile dhana kuwa lazima watoto wawe kama wazazi. Unapotaka mtoto awe kama wewe maana yake hutamruhusu kuwa yeye na hivyo kumjengea utashi wake binafsi. Hali kama hii itamfanya mtoto aidha ajaribu kuwa kama wewe au ajisikie hatia anaposhindwa kuwa kama wewe.

Ili kuwapa nafasi watoto kufanya uamuzi wenyewe, kuna haja ya kukubali ukweli kwamba nao wanaweza kuwa tofauti na wazazi. Unaweza kutaka wawe kama wewe, wafanye kazi kama mnazofanya, waishi mahali unapopataka, lakini tambua kuwa hawalazimiki kuwa nakala ya maisha ya wazazi. Unapowapa uhuru huo ni vyema ukajiuliza ni wakati upi unalazimika kuingilia kati?

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here