30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE ZA KIINGEREZA 28 ZAFUNGIWA DAR

NA CHRISTINA GAULUHANGA

  • DAR ES SALAAM

SERIKALI imezifungia shule binafsi 28 za msingi na awali, kwa kukosa sifa mbalimbali, ikiwamo uchakavu wa miundombinu ya majengo na vyoo, huku nyingine zaidi ya 100 zikiendelea kufanyiwa ukaguzi.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni mwaka mmoja tangu shule nyingine 40 za sekondari, msingi na za awali kufungiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.

Kutokana na hali hiyo, wamiliki wa shule binafsi wamelaani hatua hiyo ya Serikali, wakisema imekuwa na sura mbili.

Kwamba shule zao zinafungiwa kila mara kwa kisingizio cha ubora, huku zile za Serikali zikiwa kwenye hali mbaya zaidi, lakini hazichukuliwi hatua.

 

SHULE ZILIZOFUNGIWA

Shule zilizofungiwa zote zipo katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ambazo ni pamoja na New Generationi, Gift Academic, Comfort Life, Pwani Islamic, Mbinga Primary School, Vision Primary and Nursery School na Day Care Centre Montesory.

Nyingine ni Olivian, Makini, Real School, Aquit, Kibara, Lizzi Nursery, St. Grace Primary na Morning Star Nursery and Primary School.

Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas, jana aliliambia gazeti hili kuwa shule hizo zilifungwa katika operesheni maalumu inayoendelea ndani ya manispaa hiyo, kukagua shule zisizo na ubora na ambazo hazijasajiliwa.

Alisema katika operesheni hiyo, shule 125 za binafsi, zikiwamo 60 za msingi 65 za awali, zitakaguliwa ubora wake ili kujiridhisha kama zimekidhi viwango vinavyotakiwa na Serikali.

“Katika ukaguzi wa awali, tayari tumefanikiwa kuzifungia shule 28 ambazo baada ya kukaguliwa tumebaini wamekiuka masharti mengi, ikiwemo miundombinu ya vyoo na majengo pia,” alisema Elizabeth.

Alisema manispaa hiyo ilitoa miezi mitatu kwa wamiliki wa shule binafsi kuhakikisha shule zao zinapata usajili, lakini baadhi yao wamekuwa wajanja na wakatumia njia za panya kuwasajili wanafunzi wao kwa kutumia majina ya shule za ndugu na jamaa zao.

Elizabeth alisema walibaini mchezo huo mchafu baada ya kukuta shule imesajili wanafunzi wengi, lakini cha ajabu orodha ya wanaoendelea na masomo ni wachache.

“Baadhi ya wamiliki baada ya kuona shule zao hazina sifa za kusajiliwa, wameamua kudiriki kuwasajili wanafunzi wao katika shule za marafiki zao kisha wao kuendelea na wanafunzi wao jambo ambalo ni hatari,” alisema Elizabeth.

 

WAMILIKI SHULE BINAFSI

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la watoa elimu wasiotegemea Serikali, Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamini Nkonya, alisema kuwa hatua ya kuzifungia shule hizo si suluhisho mwafaka kwa watu binafsi waliojitolea kuwekeza kwenye sekta ya elimu.

Alisema Serikali imetengeneza sheria ngumu ya kuzibana shule binafsi bila kuangalia mchango wake kwa taifa, kwani zinapaswa kulelewa na si kufungiwa kama inavyofanyika.

Nkonya alisema shule binafsi zinawekewa sheria ngumu ili zishindwe kuendelea tofauti na zile za Serikali, huku akitaja sharti mojawapo la kuanzisha shule binafsi kwamba ni kuwa na fedha taslimu Sh milioni 60 katika akaunti.

“Kuna maeneo mengine unaweza kutumia matofali ya kuchoma na malighafi zinazopatikana kujenga shule bila kuhitaji kiasi hicho kikubwa cha fedha.

“Hatua hiyo iliyochukuliwa inaonyesha ubaguzi mkubwa, kwa sababu shule zilizofungiwa ni bora kuliko za Serikali. Ingekuwa lengo ni kuziboresha tungeelewa, lakini hii ni kutaka kuzikomoa.

“Sisi kama wadau tunafikiri na tulikwishashauri na kupeleka mapendekezo yetu, kwamba kuwepo na utaratibu wa kuzilea shule hizi kama inavyofanyika kwa vyuo vikuu. Shule moja ilelewe na nyingine na baadaye inaweza kujitegemea,” alisema.

 

SHULE ZILIZOFUNGIWA MWAKA JANA

Mwaka jana, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ilizifuta shule za awali, msingi na sekondari zaidi ya 40 katika maeneo mbalimbali nchini, ambazo hazijasajiliwa kuanzia Julai mwaka 2015.

Shule za msingi na awali zilizofungiwa ni Must Lead, Dancraig na Qunu za Mkoa wa Pwani, Brainstorm, Pax, Lassana, Grace, Rose Land na Julius Raymod, St Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde na Immaculate Heart of Mary za Dar es Salaam.

Nyingine ni St Columba, Corner stone, Dancraig, Mwalimu Edward Kalunga, Edson Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba Awali, Bilal Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance Citizen, Comrade, Dar Elite Preparatory, Golden Hill Academy na Hekima pia za Dar es Salaam.

Shule nyingine Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi Encysloped za Kagera, Hellen’s (Njombe), Joseph (Arusha),  Samandito na Maguzu za Geita.

Shule za sekondari zilizofungiwa ni Hananasif, Elu, Hocet, Safina, Fountain Gate za Dar es Salaam na Namnyaki ya Iringa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles