23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Shule za Kemebos na Kaizilege zapokea tuzo ya mshindi wa pili kitaifa kidato cha sita

Na Nyemo Malecela, Kagera

SHULE ya Kemebos na Kaizilege za mkoani Kagera zimepokea tuzo ya mshindi wa pili kitaifa mwaka 2020 katika mtihani wa kidato cha sita kutoka Wizara ya Tamisemi.

Mbali na tuzo hiyo pia walimu sita wa masomo tofauti kutoka shule hizo walipewa tuzo za walimu bora kitaifa wakati wahitimu watatu nao wakipewa tuzo za washindi bora kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Tamisemi.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abedinego Keshomshahara ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha nne na darasa la saba amesema katika miaka 14 za kuanzishwa kwa shule hizo zimefanikiwa kuchukua tuzo za Raisi katika utunzaji mazingira na upandaji miti, tuzo za Rais kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Tamisemi na Taaluma nchini.

Dk Keshomshahara alisema siri ya ushindi wa shule hizo kimkoa na kitaifa ni nidhamu waliyonayo wanafunzi katika masomo.

“Kemebos na Kaizilege ni miongoni mwa shule zenye nidhamu na taaluma inaendana na nidhamu ambayo uleta ushindi, mafanikio na ufanisi katika kila jambo, hivyo endeleeni kumtanguliza Mungu kwa kila hatua ya masomo yenu,” aliwasihi.

“Pia ili uweze kupata mafanikio katika elimu lazima uwekeze kwa kiwango kikubwa, hivyo nawapongeza kwa kuanzisha zahanati kubwa na ya kisasa ambayo imekuwa ikisaidia kuhakikisha afya za wanafunzi zinakuwa imara muda wote wawapo shuleni.”

Pia amempongeza Mkuu wa shule hizo kwa kuweka utaratibu wa kutoa motisha kwa watumishi wa shule hiyo wanaofanya vizuri katika Idara zao jambo linaloongeza ushindani na uwajibikaji kazini pamoja na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao.

Naye Meneja wa shule za Kemebos na Kaizilege, Eurojius Katiti alisema shule hizo zimefanikiwa kupeperusha vema bendera ya Mkoa wa Kagera kwa kushika nafasi za juu katika mitihani ya kitaifa kwa kuongoza kiwilaya, kimkoa na kitaifa.

“Kutokana na ushindi tulioupata mara nyingi kwa miaka mfululizo tumelazimika kuongeza uwekezaji katika miundombinu itakayowawezesha wanafunzi kupata elimu bora.

Tuzo tulizozipata zimetuongezea chachu ya kufanya vizuri na kuwekewa mikakati ya kuongeza ufahulu kwa wanafunzi kwa kutoa motisha ya zawadi kwa wanafunzi bora wanaoingia kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa na kwa walimu wa masomo ya wanafunzi waliofanya vizuri,” alieleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles