23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE ZA BWENI, MUSTAKABALI WA TABIA ZA WATOTO

Na Christian Bwaya


KUMEKUWAPO ongezeko kubwa la shule za msingi zinazotoa huduma ya bweni. Ni wazi ongezeko hilo ni matokeo ya mahitaji ya jamii. Hata hivyo, ubora wa huduma zinazotolewa kwenye shule hizo unatishia mustakabali wa watoto kitabia.

Changamoto zinazotokana na shule za bweni kwa watoto wadogo zimefanya nchi kadhaa kupiga marufuku shule za msingi kutoa huduma ya bweni. Kwa hapa jirani, Rwanda ni mfano wa nchi hizo.

Mwaka 2015 serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, iliwahi kuwatahadharisha wazazi juu ya hatari ya kuwapeleka watoto wadogo kwenye shule za bweni.

Mbali na tahadhari hiyo iliyokuwa sehemu ya maswali na majibu bungeni, hapakuwa na mwongozo mwingine wowote mahususi kwa wazazi wala wamiliki wa shule.

Wamiliki wanaendelea kutoa huduma hizo za bweni kwa watoto bila tahadhari zozote. Wazazi nao wameachwa kufanya uamuzi bila mwongozo wowote wa mamlaka zinazohusika. Makala haya yanazishauri mamlaka husika kuhusu hatua za kuchukua.

 

Mwongozo kwa wamiliki

Kwa sasa shule zinazotoa huduma ya bweni zinafanya shughuli zake kiholela. Hakuna namna nzuri ya kudhibiti utoaji wa huduma hizo shuleni.

Kwa mfano; hakuna mwongozo wa sifa za walezi wanaopaswa kuwaangalia watoto katika mazingira ya shule; uwiano wa idadi ya walezi na watoto; ukubwa wa makundi ya watoto wanaoangaliwa na walezi na mambo kama hayo.

Mamlaka zinazohusika zinahitaji kutoa mwongozo rasmi utakaowalazimisha wamiliki wa shule hizi kuzingatia vigezo. Mathalani, wamiliki walazimike kuajiri walezi wenye sifa fulani za kitaaluma zitakazowasaidia kuelewa mahitaji ya watoto kiumri. Jambo hili linawezekana kwa sababu vyuo vingi tayari vinafundisha elimu ya makuzi na malezi kwa ngazi mbalimbali.

 

Wazazi waelimishwe

Wazazi wengi hawana sababu ya msingi inayowafanya wawapeleke watoto kwenye shule za bweni. Wengi wanaamini mtoto kusoma shule ya bweni ni ufahari. Wengine wanafikiri mafanikio ya mtoto kitaaluma hayawezi kupatikana kwenye mazingira ya nyumbani. Wazazi hawa waelimishwe.

Tunahitaji wazazi waelewe umuhimu wa ukaribu na mtoto katika umri mdogo. Kwamba si sahihi kumpeleka mtoto kwenye mazingira ya mbali na familia. Kila inapobidi, watoto wasome karibu na wazazi. Mamlaka zitoe elimu kwa umma kuhusu jambo hili.

Kadhalika, wazazi waelimishwe umuhimu wa kujenga mazingira sisimushi kwa watoto nyumbani. Badala ya kufikiria shule ya bweni, mzazi aelimishwe kuwa akihakikisha mazingira ya nyumbani yanamsaidia mtoto kujifunza bila vikwazo hatakuwa na sababu ya kumpeleka mtoto mbali. Mamlaka zisaidie kutoa elimu hii kwa wazazi.

Utafiti

Huduma za bweni kwa watoto wadogo zimefanyiwa tafiti nyingi. Bahati mbaya tafiti hizi zinazofahamika zimefanyika katika nchi zilizoendelea. Hadi mwaka 2015, kwa mfano, hapakuwapo na utafiti wowote wa huduma hizi hapa nchini.

Utafiti huo uliokuwa sehemu ya tunuku ya kitaaluma, ulifanyika kama ‘pima joto’ ya kujua hali halisi. Katika mazingira hayo, unahitajika utafiti mpana utakaojumuisha shule nyingi ili matokeo yake yasaidie kuelewa hali ya shule hizi kitaifa.

Kwa sababu hiyo, ni vyema mamlaka zinazohusika zikaona uwezekano wa kufanya utafiti mpana wa kitaifa utakaosaidia kujua kinachoendelea kwenye shule hizi. Hii itazisaidia mamlaka husika kufanya maamuzi ya kisera yenye tija kwa wazazi na jamii kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles