Na GUSTAPHU HAULE-PWANI
SHULE ya Sekondari Tumbi iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, imefanya sherehe ya kumpongeza mwanafunzi wake Agape Mwalimu, ambaye ni miongoni mwa wasichana waliofanya vizuri kutoka shule za kata.
Shule hiyo ya Tumbi katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, ilikuwa ya 30 kati ya 129 kimkoa na ya 840 kati ya shule 3,908 kitaifa.
Wanafunzi wa shule hiyo waliofanya mtihani ni 165, na kati yao watano walipata daraja la kwanza, 29 daraja la pili, 45 daraja la tatu, 66 daraja la nne na 20 walipata sifuri.
Kati ya waliopata daraja la kwanza, Agape alipata daraja la kwanza na ponti nane.
Sherehe ya kumpongeza Agape ilifanyika juzi shuleni hapo ikiongozwa na Mkuu wa Shule hiyo, Fidelis Haule na kuwashirikisha walimu na wanafunzi.
Mbali na kumpongeza mwanafunzi huyo, pia ilikuwa sehemu ya kuwapongeza wengine wa kidato cha tatu waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha pili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Haule alisema amefurahishwa kuona mwanafunzi wa kike kutoka shule yake anaongoza kitaifa kwa kupata alama za juu jambo ambalo linatia moyo kwa walimu na hata kuchochea maendeleo ya elimu shuleni hapo.
Haule, alisema kutokana na hali hiyo, wameona ni vyema wakafanya sherehe ya pamoja na mwanafunzi huyo mbele ya waliobaki shuleni hapo ili kuwapa molari wa kusoma zaidi, huku akisema lengo ni kupata matokeo mazuri zaidi mwakani.
Alisema mwaka jana walimzawadia mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza pointi saba na kuongoza kitaifa kwa shule za kata na mwaka huu wamepata msichana na utaratibu huo utakuwa endelevu kwa watakaofanya vizuri.
Haule alisema ana imani mwaka ujao shule itapata ufaulu mzuri kwakuwa walimu wamejipanga kikamilifu kufundisha huku akiwataka wanafunzi kusoma kwa bidii na hata kuongeza nidhamu wakiwa shuleni hapo.
Kwa upande wake, Agape akizungumza mara baada ya kupokea zawadi aliyoandaliwa, alimshukuru mkuu wa shule hiyo na walimu wake kwa kutambua umuhimu wa kumpongeza kwa matokeo hayo.
Agape aliwataka wanafunzi waliobaki shuleni hapo, hususani wa kike, kujiepusha na vitendo viovu na badala yake wasome kwa bidii ili waandae vizuri maisha yao ya baadae.