27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Shule iliyokuwa ikidharauliwa yawa ya kwanza kitaifa

PICHA WANAFUNZI MAABARA SEKONDARY.
Wanafunzi wakiendelea na masomo maabara.

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

JULAI 15 mwaka huu, Baraza la Mitihani nchini (NECTA), lilitangaza matokeo ya kidato cha sita (ACSEE), ambayo pamoja na mambo mengine yameonesha wasichana wanaongoza kwa ufaulu wa asilimia 98.59 dhidi ya wavulana waliofaulu kwa kiwango cha asilimia 97.55.

Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, yamethibitisha au kupigia mstari mashairi ya wimbo wa mwanamuziki wa nyimbo za injili, Rose Muhando, unaosema; “Wanaokudharau siku moja watakusalimia kwa heshima.”

Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na historia ya Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopo Kijiji cha Kisimiri Chini, Kata ya Uwiro wilayani Arumeru mkoani Arusha, kuchukiwa na kuonekana shule ya adhabu kwa walimu na wanafunzi.

Ikiwa na kidato cha kwanza mpaka cha sita kwa wanafunzi mchanganyiko, shule hiyo ya kata ipo kaskazini mwa Mlima Meru mkoani Arusha, ambapo ili iwe rahisi kufika yakupasa kupita barabara inayopita ndani ya Hifadhi ya Arusha kutokea Mji wa Usa River.

Mazingira ni magumu lakini pia miundombinu ya kukufikisha shuleni ni mibovu hasa kuwapo kwa makorongo ambayo nyakati za masika hupitisha maji na kuongeza ugumu wa kufika shuleni hasa baada ya kuwa umewasili katika mji wa Ngarenanyuki.

Shule hiyo ipo katika kata mpya ya Uwiro yenye vijiji viwili, Kisimiri Chini ilipo shule pamoja na Kijiji cha Kisimiri Juu ambacho ni maarufu kwa wananchi wake kujishughulisha na kilimo cha bangi ‘Kitu cha Arusha’.

MWALIMU MKUU

Wakati Kata ya Uwiro ikikabiliana na changamoto ya ulimaji bangi kwenye kijiji chake kimoja, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisimiri, Emmanuel Kisongo, amefanikiwa kuandika historia nyingine kwa Kijiji cha Kisimiri Chini katika sekta ya elimu.

Mwalimu huyo anayejulikana kwa jina la utani la ‘Chopa’ anasema, kidato cha sita kulikuwa na wanafunzi 63 ambapo wanafunzi 50 wamepata daraja la kwanza na wanafunzi 13 daraja la pili.

Anasema baada ya kufika shuleni hapo mwaka 2006 akitokea Sekondari ya Galanos na Segera za Tanga, alikuta ikiwa na walimu tisa huku baadhi wakitajwa kuikimbia kutokana na kuonekana kama shule ya adhabu.

Wakati akihamia shuleni hapo, anasema alikuta wanafunzi 1,800 wa kidato cha kwanza mpaka cha sita, ambapo kwa kidato cha sita pekee alikuta wanafunzi sita tu.

“Wanafunzi sita niliowakuta niliwaita “Six Form Six” nilianza nao na ndani ya miezi sita nilifanya mapinduzi na tukafanikiwa kuwa wa pili kitaifa.

“Niliendelea kuwaza nitapata wapi walimu, nilienda ofisi za elimu mkoani kuomba walimu nikaambiwa siwezi kupewa kwani wengi hawaipeindi Kisimiri.

Kisongo anayeendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PHD), anasema kitendo cha kuikuta shule hiyo ikiwa kwenye hali ngumu kilimuumiza hatua iliyomfanya ajiwekee vigezo vya kufikia mafanikio.

“Niliogopa kwa kuona nimeachiwa shule peke yangu. Nilisema moyoni kwamba hapa ndipo natakiwa kulipa deni kwa Watanzania.

“Tulianza kuimarisha maabara kupitia kwa marafiki na wadhamini wetu. Na kwa miaka 10 niliyokaa pale sijawahi kupewa fedha na Serikali hata ya kujenga darasa.

“Tumefanya kwa nguvu za wafadhili kama Professa Emil Karafiat, wa nchini Uswis aliyekulia Kisimiri, hawa wametusaidia ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu,” anasema Mwalimu Kisongo.

Anasema moja ya mambo yaliyokuwa yakimuuza kwa shule hiyo na zingine za kata ni kudharaulika na kuitwa shule za Yeboyebo.

Mwalimu Kisongo anaeleza kwamba shule hiyo ilianzishwa mwaka 2002 kwa kidato cha kwanza na ilipofika mwaka 2006 kidato cha sita kilianzishwa.

Anasema ilipofika mwaka 2011, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi iliamua kuipandisha hadi kuwa shule maalumu kwa upande wa kidato cha tano na sita, hatua anayoielezea kuwa ilichangiwa na matokeo mazuri na si vinginevyo.

Mwalimu Kisongo alisoma katika Shule ya Msingi Salare, Kata ya Pahi wilayani Kondoa mkoani Dodoma na baada ya kumaliza darasa la saba alijiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Dodoma kuanzia mwaka 1985 hadi 1988.

Baada ya hapo alijiunga na Mkwawa Complex kwa masomo ya kidato cha tano na sita akisoma Kemia na Hisabati (CM). Ambapo akiwa hapo aliweza kuimarika kutokana na kusoma na walimu wakifundisha bila mzaha.

“Pale tulisoma na kufanya mitihani vizuri, tulipelekwa tukiwa na uwezo wa daraja la kwanza na la pili, ndio tulikwenda kusomea ualimu tofauti na siku hizi. Sisi tulikuwa na uwezo wa darasani na kiutendaji,”anasema Mwalimu Kisongo.

Anasema alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa chini ya Professa Bangu kisha kuendelea na masomo ya Shahada ya Pili  ya Ualimu na Uongozi katika Chuo Kikuu cha Arusha.

“Nimefundisha muda mfupi, nimekuwa kwenye utawala na kuongoza. Nikiwa darasani nimeweka rekodi Mkwakwani Sekondari ambapo darasa langu kwa somo la Hisabati liliwahi kuwa la kwanza kitaifa.

“Hii ni tabia yangu ya kuvunja rekodi. Kila siku huwa natamani kuvunja rekodi nilizoweka nyuma,” anasema.

JINSI ALIVYOPOKEA MATOKEO

Mwalimu huyo anasema akiwa Dar es Salaam kwa shughuli zingine alipigiwa simu na mmoja wa wanafunzi wake na kumjulisha kuhusu matokeo.

“Nilikuwa ofisini kwa Waziri wa Elimu, Professa Joyce Ndalichako. Mwanafunzi wangu akapiga simu na kuniambia tayari tumeua. Nilifurahia na kwa kuwa nilikuwa kwa waziri ilibidi nijibane. Ila simu zangu zilipigwa na kuisha chaji zikazimika,” anasema Mwalimu Kisongo.

MWALIMU WA TAALUMA

Kwa upande wake Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Valentine Tarimo, anasema matokeo hayo yamewapa ari ya kufanya kazi zaidi kupitia oparesheni walioyoianzisha ya Kisimiri Sawazisha.

“Tumejipanga mwaka huu O- Lavel hatutakuwa na sifuri na A- Lavel pia unajua taaluma ni mipango na hapa Kisimiri hatuhitaji fedha tunahitaji akili.

“Tuna walimu 68, asilimia 90 wanaishi eneo la shule. Hapa tuna maabara tano, changamoto kubwa ni ubovu wa barabara na ukosefu wa uzio,” anasema Mwalimu Tarimo mwenye Shahada ya Uzamili ya Sera na Mipango katika Ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere Uganda.

Anasema katika matokeo ya mwaka 2008 walifanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa, 2009 nafasi ya 12, 2010 nafasi ya 19, 2011 nafasi ya tatu, 2012 nafasi ya tano, 2013 nafasi ya tatu, 2014 nafasi ya nane na 2015/16 wakafanikiwa kuwa wa kwanza kitaifa.

Shule 10 bora zilizotangazwa ni Kisimiri Arusha, Feza Boys na Gilrs za Dar es Salaam, Alliance Gilrs ya Mwanza, Marian Boys ya Pwani, Kibaha ya Pwani, Mzumbe Morogoro, Ilboru ya Arusha, Tabora Boys Tabora na Tandahimba iliyopo Mtwara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles