Shirika la Nyumba lamtikisa Mbowe

0
798
Wafanayakazi wa kampuni za udalali wakitoa vyombo vya Kampuni ya Free Media inayochapisha gazeti la Tanzania Daima kwa madai ya kushindwa kulipa deni la kodi ya pango, Dar es Salaam jana.
Wafanayakazi wa kampuni za udalali wakitoa vyombo vya Kampuni ya Free Media inayochapisha gazeti la Tanzania Daima kwa madai ya kushindwa kulipa deni la kodi ya pango, Dar es Salaam jana.
Wafanayakazi wa kampuni za udalali wakitoa vyombo vya Kampuni ya Free Media inayochapisha gazeti la Tanzania Daima kwa madai ya kushindwa kulipa deni la kodi ya pango, Dar es Salaam jana.

NA CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), jana limevamia na kutoa vifaa vyote vinavyotumiwa na Kampuni ya Free Media, inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari katika jengo lililopo makutano ya Mtaa wa Mkwepu na Makunganya Jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo zilizopo ofisi Gazeti la Tanzania Daima na Club Billinas linadaiwa kumilikiwa na familia ya marehemu Aikael Mbowe ambaye ni baba mzazi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, chini ya wakurugenzi, Dadle Aikael na Lilian Mtei.

Hatua hiyo imekuwa wiki moja baada ya NHC kutangaza orodha ya wadaiwa sugu akiwemo Mbowe, ambaye anadaiwa kushindwa kulipia kodi ya pango zaidi ya Sh bilioni 1.172 ambayo ni malimbikizo tangu miaka ya  1990.

Jengo hilo ambalo pia linajumuisha ukumbi maarufu wa Bilicanas ulivamiwa jana saa moja asubuhi ambapo Kampuni ya Udalali ya Fosters Auction Mart wakiongozwa na Joshua Mwituka waliingia kwenye ofisi hizo na kutoa nje vifaa vyote vinavyohusika kuandalia magazeti hayo.

Hata hivyo madalali hao walishindwa kuondoa vifaa vya muziki katika ukumbi wa Bilicanas, ikiwaida kuwa  vimefungwa kwa ustadi mkubwa na mafundi kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo ilipofika mchana jana mafundi walifika katika eneo hilo na kuendelea kufungua vifaa vya muziki vilivyopo ndani ya ukumbi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, Meneja wa Kitengo cha Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japheth Mwanasenga,  alisema mpangaji wao anadaiwa kodi kwa zaidi ya miaka 20 ambapo taratibu za kudai deni la awali zilifanyika, lakini mteja huyo amekuwa akikaidi.

Alisema baada ya kukaidi kwa muda mrefu walimpa siku saba awe amehamisha vitu vyake ndani ya jengo hilo, lakini hadi jana wakati kazi hiyo inaanza hakuna kilichoondolewa.

“Tukio hili halihusiani na mambo ya kisiasa, mmiliki wa jengo hili ni mdaiwa sugu kama walivyo wengine…hivyo kwa sababu amekaidi agizo letu la awali la kuhama kwa hiari tumeanza kwa kumuhamisha halafu tunampa siku 14 awe amelipa deni letu vinginevyo vitu vyake tutaviuza na kupiga mnada,”alisema Mwanasenga.

Alisema mbali na Mbowe pia wapo wadaiwa wengine sugu zikiwemo taasisi za Serikali na watu binafsi, lakini kwa kuanza wameanza na Mbowe.

Naye dalali Mwituka alisema sheria ya mwaka 2005 inampa mamlaka ya kumwondoa mpangaji iwapo ameshindwa kulipa kodi.

“ Sisi tunachofuata ni agizo tulilopewa na mteja wetu ambaye ni NHC. Baada ya kutoa vyombo nje tutasikiliza kama tunatakiwa tupige mnada au laa,”alisema Mwituka.

Kwa upande wake, Mwansheria wa NHC Kitengo cha Madeni, Mariam Ngulla, alisema shirika hilo limechukua uamuzi huo baada ya kufuata taratibu zote ikiwemo kumpa notisi mdeni wao.

Hata hivyo kuna utata ulioibuka kuhusu uhalali unaodaiwa kuwa Mbowe anamiliki hisa asilimia 75 katika jengo hilo na NHC asilimia 25, ambapo mwanasheria huyo alisema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo.

“ Zipo taratibu za kisheria ambazo zimefanyika hivyo sisi tunachofahamu anayeondolewa ni mpangaji wetu mengine hatuwezi kuyazungumza hapa leo,”alisema Mariam.

MTANZANIA lilishuhudia mali za ofisi zilizokuwepo ndani ya jengo hilo zikiwa zimelundikwa nje huku walinzi kutoka Kampuni ya Diamond wakiendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Mbali na walinzi hao, wafanyakazi wa Kampuni ya Free Media na Club Bilicanas pia walikuwa wakirandaranda nje ya jengo hilo, huku wengine wakijaribu kuweka sawa vifaa vyao.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alimtaja Mbowe na taasisi nyingine binafsi na za Serikali kuwa ni wadaiwa sugu wa shirika hilo.

Awali, ilidaiwa kuwa Mbowe alikuwa na ubia na NHC katika jengo hilo, lakini hivi sasa ubia huo umevunjwa hivyo itabaki kuwa mali ya umma na kama atashindwa kulilipa deni hilo hatua za kisheria zitafuatwa ikiwemo kukamatwa kwa mali zake.

“Pale Bilicanas mwanzo tulikuwa na ubia, lakini tumeuvunja na sasa NHC tutaendeleza wenyewe eneo hilo, hivyo kama Mbowe hatalipa basi sheria zitachukuliwa na kama atalipa ataachwa aendelee kuwa mpangaji na deni hilo kwa mkupuo,” alisema Mchechu.

Kauli ya Mbowe

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbowe alisema alipata taarifa za watu kuingia katika jengo hilo na tayari ameanza mchakato wa kisheria.

“Mawakili wangu wapo mbele ya Jaji. Ninajua NHC wametuma mabaunsa wao na nitakwenda kudai damage (hasara),” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema jambo hilo lilipangwa kwa makusudi, kwani NHC walijua leo (jana) wangefanya maandamano ili na wao watimize azma yao.

“Ninajua jambo hili linamwelekeo wa kisiasa nami nimejipanga kusimamia ukweli kupitia mahakama,” alisema Mbowe.

Wadaiwa wengine

Mbali na NHC kuanza kuondoa vitu katika jengo hilo la Mbowe Hotel, wadaiwa wengine sugu walitajwa kuwa ni Wizara ya Uchukuzi ambayo inadaiwa Sh bilioni 2.7, Wizara ya Afya, Sh bilioni 1.3, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Sh bilioni 1.1, Tume ya Utumishi wa Umma, Sh milioni 109.9 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Sh milioni 631.8.

Wengine wanaodaiwa na shirika hilo ni Benki ya Azania Sh milioni 161.9, A. D. Investment Limited Sh milioni 155.4, Palace Hotel LTD Sh milioni 128.1.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here