PRETORIA, AFRIKA KUSINI
CHAMA tawala cha African National Congress (ANC), jana kiliitisha kikao cha dharura kujadili hali ya baadaye ya Rais Jacob Zuma, baada ya mazungumzo ya juzi usiku kushindwa kumshawishi ajiuzulu.
Zuma, ambaye yuko madarakani tangu mwaka 2009, kutokana na kashfa za ufisadi amekuwa akizidi kubanwa kumtaka ajiuzulu tangu nafasi yake ya kuiongoza ANC ilipochukuliwa na makamu wake, Cyril Ramaphosa Desemba mwaka jana.
ANC iliitisha kikao cha Kamati ya Taifa ya Utendaji kukutana katika makao makuu ya chama hicho, Luthuli House jijini Johannesburg kwa majadiliano.
Ili chama hicho kiweze kumlazimisha Zuma kujiuzulu nafasi yake ya rais wa nchi, kamati hiyo italazimika kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ya Taifa, ikiwa ni chombo chake kikuu cha uamuzi, kupiga kura kumwondoa Zuma.
Maofisa sita wa ngazi ya juu wa ANC, walikutana na Zuma usiku wa juzi katika makazi yake mjini Pretoria, lakini hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu kikao hicho.
Kiongozi wa upinzani, Julius Malema, mwanachama wa zamani wa ANC, alisema Zuma amegoma kujiuzulu.
“Amekataa kujiuzulu na aliwaambia wachukue uamuzi kumwondoa iwapo wanataka kufanya hivyo, kwa sababu hajafanya lolote baya kwa nchi,” Malema aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Zuma ametengwa na washirika wake muhimu tangu Ramaphosa achaguliwe kuongoza chama pekee kuiongoza Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa Wazungu wachache mwaka 1994.
Ramaphosa (65) yuko katika nafasi nzuri ya kuwa rais ajaye na amekuwa akiingiza ushawishi wake ili Zuma aondolewe madarakani.
Zuma hajasema iwapo atajiuzulu kwa hiari kabla ya muda wake wa muhula wa pili kumalizika mwakani.
Vyama vya upinzani na baadhi ya wanachama wa ANC, wanataka aondoke kabla ya hotuba ya hali ya taifa hilo katika Bunge, iliyopangwa kutolewa hapo Alhamisi.
Zuma anastahili kusalia madarakani hadi uchaguzi wa mwakani, lakini chini yake chama kimepoteza umaarufu, uchumi ukidorora na tuhuma za rushwa zikikithiri.
Kwa sababu hiyo, viongozi wanataka aondoke mapema kabla ya uchaguzi huo, kusafisha taswira ya chama mapema na kukijengea upya sifa yake.