25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Shida ya maji Kibakwe yabaki historia

Ni baada ya kusainiwa mradi wa Sh bilioni 4.3

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wananchi wa kata ya Pwaga wanatarajia kuanza kunufaika na mradi mpya wa maji baada ya serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa maji kupitia Mkandarasi Pioneer Building Limited.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, George Simbachawene akishuhudia uwekaji wa saini kati ya Mkandarasi Pionner Buiding Limited, Meneja wa Ruwasa, Cyprian Warioba na Muwakilishi wa Meneja wa RUWASA Mkoa, Priscilla Mkilanya.

Hayo yamefanyika wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, George Simbachawene alipokabidhi nakala ya Mkataba wa Ujenzi wa mradi huo maji unaotarajia kukamilika baada ya mwaka mmoja, kwa diwani wa kata ya Pwaga, Wilfred Mgonela katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Pwaga jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

“Nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha nyingi kiasi cha Sh bilioni 4.3 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ya maji katika kata ya Pwaga utakaosaidia vijijji vitano vya, Maswala, Itende, Ng’onje, Mungui na Pwaga.

“Lazima tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi wa maji na kwa uwazi ili wote tuwe na uwezo wa kuona kilichopo na kuondoa mianya ya vitendo vya udanganyifu katika utekelezaji wake.

“Mradi huu utatoa ajira nyingi kwa wananchi ambazo zitasaidia kujenga uchumi wa kata ya Pwaga,” amesema Simbachawene.

Aidha, Waziri ametoa wito kwa Mkandarasi Pioneer Building Limited kutekeleza mradi wa maji kwa kasi ili watu waanze kupata huduma ya maji.

Amehimiza mfumo wa uongozi, wa maji kata ya Pwaga kusukwa upya ili uweze kusimamia vizuri mradi wa maji na uendane na sera pamoja na sheria ya maji.

Naye diwani wa kata ya Pwaga, Wilfred Mgonela ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha za Utekelezaji wa mradi wa maji.

“Naomba watendaji na wananchi tushirikiane kusimamia vyema mradi ili yasije yakajitokeza mapungufu katika utekelezaji wa mradi,” amesema Mgonela.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mwl. Jakson John amesema kukamilika kwa mradi wa maji Pwaga utasaidia afya za watu kuimarika.

“Sisi tunaosimamia sekta ya elimu kwa upande wa shule ya Msingi tunawanafunzi 5,000 ambao watanufaika na mradi huu wa maji,” amesema.

Katika taarifa yake Meneja wa RUWASA Halmashauri ya Mpwapwa, Injinia Cyprian Warioba amesema shughuli zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Rufu, ujenzi wa tenki moja lenye uwezo wa kuhifadhi lita  500,000 za maji litakalojengwa kijiji cha Ng’onje, kutakuwa na ujenzi wa tenki la pili la maji wa lita 50,000 litakalo jengwa kijiji cha Itende.

“Kutakuwa na ujenzi wa Ofisi moja kwa ajili ya uendeshaji na uendelevu wa mradi itakayotumiwa na viongozi watakaosimamia zoezi zima la uendeshaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na vituo vya kuchotea maji 27 pamoja na Marambo manne ya kunyweshea mifugo.

“Tunakusudia kukamilisha mtandao wa bomba jumla ya km 61, ambazo km 15 ni kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki la Ng’onje  na km 43 ni mtandao kwa maeneo yote kwa maana ya vijiji vyote vinavyohusiana na mradi Itende, Pwaga, Mungui pamoja na Maswala,” alisema Injinia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles